Saturday, December 20, 2014

WAPOTEZA MAISHA KWA MAMBO YA KIMAPENZI NA USHIRIKINA



Steven Augustino na Abbas Mlanya,
Ruvuma.

WATU wawili wamefariki dunia mkoani Ruvuma, katika matukio mawili tofauti yaliyotokea wilayani Tunduru na Namtumbo mkoani humo, ambapo la kwanza linasababishwa na wivu wa kimapenzi na lingine linahusishwa na mambo ya ushirikina.

Baadhi ya mashuhuda wa tukio lililotokea wilayani Tunduru, walisema kuwa marahemu aliyetambuliwa kwa jina la Yusuph Jafari ambaye amehamia wilayani humo, akitokea wilaya ya Masasi alikuwa kinara wa kutembea na wake za watu na baadaye kuuawa na watu wasiojulikana.

Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Ruvuma, ASP Mihayo Msikhela alisema kuwa tukio la kwanza lilitokea  Disemba 16 mwaka huu katika kitongoji cha Naunditi kijiji cha Majimaji, kilichopo kata ya Muhuwesi wilayani humo.


Alisema katika tukio hilo Yusuph jafari (54) alikutwa akiwa amefariki dunia nje ya nyumba yake, huku akiwa amekatwakatwa kwa mapanga na mwili wake ukiwa umetelekezwa nje ya nyumba yake.

Kuhusu tukio la pili ambalo lilihusishwa na mambo ya kishirikina lililotokea wilayani Namtumbo, ambapo kamanda Msikhela nalo amethibitisha likimhusisha mzee mwenye umri wa miaka 64 aliyetambuliwa kwa jina la Yasin Fussi.

Tukio hilo imeelezwa kuwa lilitokana na wananchi kuchukua sheria mkononi wakimtuhumu kikongwe huyo, kumpoteza mtoto wake katika mazingira ya kutatanisha kwa njia za ushirikina.

Msikhela alifafanua kuwa mzee huyo, aliuawa akituhumiwa kumficha mtoto wake aliyetajwa kwa jina la Kassim Fussi anayedaiwa kutoweka  Disemba 14 mwaka huu.

Alisema baada ya tukio la kutoweka kwa kijana huyo wananchi walimwita mzee huyo na kumhoji juu ya tukio hilo, lakini hakutoa maelezo yoyote hali ambayo iliwatia shaka na hasira iliyosababisha kuchukua maamuzi hayo magumu.

Kufutia hali hiyo Jeshi la Polisi linawaomba wananchi wenye taarifa juu ya matukio hayo, kutoa ushirikiano kwa kuwataja wahusika ili waweze kukamatwa na kutoa nafasi kwa vyombo vya sheria, kuchukua mondo wake.

No comments: