Monday, December 22, 2014

KAYOMBO ALALAMIKIWA NA WAPIGA KURA WAKE KWA KUMTETEA MKURUGENZI MTENDAJI NA MKUU WA WILAYA YA MBINGA, WASEMA MWAROBAINI WAKE UCHAGUZI MKUU MWAKANI

Gaudence Kayombo.
Na Kassian Nyandindi,

Mbinga.

BAADHI ya Wakazi wa mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, wamemtaka Mbunge wa jimbo la Mbinga, Gaudence Kayombo kufuta kauli zake anapokuwa akihutubia wananchi katika majukwaa ya kisiasa na kujenga hoja za kuwatetea Mkurugenzi mtendaji Hussein Ngaga na Mkuu wa wilaya hiyo, Senyi Ngaga kwamba ni viongozi wazuri na wameleta maendeleo makubwa wilayani humo.

Sambamba na hilo wananchi hao ambao ni wapiga kura wake, wamesema kuwa kauli za Kayombo kuwatetea viongozi hao ni sawa na kujichimbia kaburi kwa kupoteza nafasi aliyonayo, katika uchaguzi mkuu ujao ambao unatarajiwa kufanyika mwakani kwa nafasi ya kumchagua Rais, Wabunge na Madiwani.

Walifafanua kuwa wanamshangaa Mbunge huyo amekuwa akiwasafisha viongozi hao wawili kwamba wanafanya vizuri, wakati maendeleo mengi yaliyofanywa wilayani humo yamefanywa na viongozi wenzao waliowatangulia na sio wao ambao wamefika hapa wilayani wanamuda mfupi na hakuna jambo jipya la maendeleo walilobuni na  kuweza kujivunia   kwa wananchi wakati mengi yaliyopo wanayoyaendeleza ni yale ambayo yalifanyiwa ubunifu na viongozi wenzao waliowatangulia.

Hayo yalisemwa jana na wakazi wa mji wa Mbinga kwa nyakati tofauti, mara baada ya Mbunge Kayombo kumaliza kuhutubia katika viwanja vya soko kuu mjini hapa, kwenye mkutano wa hadhara ambao uliandaliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani humo kwa ajili ya kushukuru wapiga kura wake kukipatia viti vingi vya nafasi ya Wenyeviti wa vitongoji, katika chaguzi za serikali za mitaa zilizofanyika hivi karibuni. 


“Sisi tunamshangaa sana huyu Mbunge, anasimama jukwaani na kuanza kumsifia mkurugenzi na mkuu wake wa wilaya, ambao dhahiri wameshindwa kuiongoza wilaya hii, kila kukicha wao wanaendekeza migogoro na wafanyakazi wenzao na kufikia hatua serikali kutumia fedha nyingi za walipa kodi kuleta tume kuchunguza mambo ya kijinga ambayo yamesababishwa na hawa watu”, walisema.

Aidha wananchi hao ambao walionekana kukerwa na kauli za Bw. Kayombo, walisema wana kila sababu za kumnyoshea kidole kwani yeye ndiye anayelea matatizo yanayoendelea hapa wilayani Mbinga ambayo yanahatarisha ustawi wa maendeleo ya wananchi wake, kwani hadi sasa ameshindwa hata kukemea na kusimama katikati ili kutenda haki badala yake anaonekana kuegemea upande wa mkurugenzi na mkuu wa wilaya hiyo.

Wengi walikuwa wanahoji na kusema kwamba, matendo anayoyafanya Mbunge huyo kwa kukumbatia uozo huu unaoendelea kutafuna kizazi hiki cha wanambinga ni dhambi ambayo itakuja kumtafuna baadae hapa hapa duniani, kutokana na watu wengi wamekuwa wakisikitika juu ya mwenendo mbaya anaoufanya wa kulea na kuficha mapungufu ya vigogo hao hapa wilayani ambayo wamekuwa wakiyafanya na kuudhi wananchi.

“Huyu Mbunge tunamashaka naye tumekaa naye vikao vingi na kumweleza matatizo ya hawa anaowatetea leo, lakini hataki kuelewa sasa asubiri mwarobaini wake uchaguzi mkuu ujao mwakani, kwa sababu tumechoka viongozi anaowasifia kila kukicha wamekuwa wakizalisha migogoro ambayo haina tija kwetu…………” 

Pamoja mambo mengine walieleza kuwa, ni vyema serikali ikasimama kidete ikatenda haki na kuingilia kati juu ya matatizo na migogoro iliyopo kazini kati ya vigogo hao wa wilaya, na wafanyakazi wenzao wa ngazi ya chini katika halmashauri ya Mbinga ili kuweza kunusuru ustawi wa maendeleo ya wananchi wa wilaya hiyo.

Waliongeza kuwa hawaoni sababu kwa serikali kuendelea kumfumbia macho Mkurugenzi Bw. Ngaga na Mkuu wa wilaya Bi. Ngaga, ambao wamekuwa wakitengeneza mifarakano kila kukicha badala ya kubuni maendeleo.

No comments: