Monday, December 1, 2014

MBINGA WANASHUGHULIKA KUKOMOA WANANCHI BADALA YA KUSIMAMIA MAENDELEO, AGIZO LA RAIS KIKWETE UJENZI WA MAABARA UTATA MTUPU

Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Na Kassian Nyandindi,


SIKU zote misingi ya taifa linalojali maisha ya wananchi wake ni ujenzi bora wa elimu, afya na miundombinu inayokuza uchumi huku viongozi wake katika eneo husika hutakiwa kuwa makini, kujenga mshikamano na kuacha migogoro ya hapa na pale.

Wahenga wetu husema, ukiona kiongozi muda mwingi amekuwa akiendekeza migogoro basi tambua kwamba, mahali pale ameshindwa kutawala na maendeleo hayawezi kupatikana badala yake serikali, inashauriwa kuchukua hatua za haraka katika kunusuru hali hiyo ili wananchi wake wasipate mateso.

Kinyume chake kukosekana kwa kiongozi wa kweli na asiyejali utawala bora au maslahi ya wananchi, kunanyima watu fursa ya kufanya maamuzi sahihi kuhusu rasilimali zao, ikiwemo hata kujiondoa katika lindi la umasikini unaonuka.

Popote pale kiongozi wa namna hii, ni sawa na kusema ni kiongozi muflisi ambaye hutambulika muda mwingi kupenda kuruhusu mianya ya rushwa kutawala kila kona, hasa wakati wa utoaji wa huduma muhimu kwa wananchi anaowaongoza.

Katika makala haya napenda kuelezea juu ya kilio cha baadhi ya wananchi wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, dhidi ya Mkuu wao wa wilaya Senyi Ngaga na Mkurugenzi wake Hussein Ngaga, jinsi gani wanavyoiyumbisha wilaya hiyo na kufikia hatua wananchi kukosa imani nao.

Nimefikia hatua ya kuliweka jambo hili hadharani kutokana na mambo kadhaa yanayokera wananchi ambayo viongozi hawa, wamefikia sasa kuchukiwa na watu wanaowaongoza kutokana na kile kinachoelezwa kuwa kupenda kufanya mambo ambayo hayana msingi katika mustakabali mzima, wa maendeleo ya wananchi wa wilaya hiyo.

Jambo la kwanza, kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali ambavyo vimetoa ushirikiano wa karibu kwa mwandishi wa makala haya, vimeeleza kuwa mkuu wa wilaya hiyo ameshindwa kukemea mgogoro ambao unaendelea kufukuta kwa muda mrefu kati ya mkurugenzi huyo na afisa elimu msingi wa wilaya hiyo, Mathias Mkali.

Aidha wanaongeza kuwa licha ya afisa elimu huyo kuonekana kufanya kazi zake vizuri katika kuboresha kiwango cha taaluma wilayani humo, cha kushangaza viongozi hao wamekuwa wakimpiga vita pasipo sababu yoyote ya msingi na kusababisha kuwepo kwa tabaka kubwa, ambalo linaitafuna wilaya kwa kurudisha nyuma maendeleo katika sekta hiyo muhimu.

Wanasema mkuu wa wilaya Ngaga, kukaa kwake kimya pamoja na serikali kukemea migogoro kazini huenda akawa amejenga maslahi yake binafsi, na kusahau jukumu alilopewa na Rais Jakaya Kikwete, wakati anamteua kwenda kutumikia wananchi wa wilaya hiyo kwa kuzingatia kuepuka misingi ya itikadi, rangi au dini na mambo mengine ambayo hayana tija katika jamii.

Wengi kwa nyakati tofauti wanasema, vitendo vinavyofanywa na mkurugenzi huyu huku mkuu huyo wa wilaya kutoingilia kati na kukemea, ni sawa na kushughulika kukomoa wananchi badala ya kubuni na kusimamia maendeleo kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.

Senyi Ngaga namfahamu vizuri, ni dada yetu ambaye wananchi wa Mbinga tulikuwa na imani naye katika kujenga mshikamano wa kuweza kusukuma mbele gurudumu la maendeleo, lakini kwa haya yanayoendelea sasa anakatisha tamaa wananchi anaowaongoza. 


Wananchi wamefikia hatua ya kuiomba serikali kuingilia kati juu ya tatizo hili ambalo linaonekana kuwa sugu, ili kuweza kupata suluhu katika sekta hiyo muhimu ya elimu ambayo sasa kuna dalili tosha za kushuka kwa elimu wilayani humo, kutokana na mgogoro huo kufikia hatua mbaya. 

 Nakumbuka mnamo mwezi Juni 1990 aliyekuwa Katibu mkuu wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) ambao baadae umekuwa umoja wa Afrika (AU) Edem Kadjo  alisema, “Waafrika kimsingi wanachohitaji ni mambo makuu matatu………uwajibikaji, uwazi na ushiriki kamilifu katika mambo ya kimaendeleo.

Hivyo basi, viongozi kutozingatia mambo haya matatu huenda kukasababisha hali ngumu ya maisha kwa wananchi wa eneo husika au taifa kwa ujumla, na kujiandikia historia mbaya itakayowafanya sisi watawala hususani katika wilaya hii, kwa wakati huo kutotamani kuandikwa hata kwenye kumbukumbu.

Siku zote nimekuwa nikijiuliza kwamba, kibuli hiki kwa mkurugenzi huyu wa Mbinga kila kukicha kulumbana na viongozi wenzake wa ngazi ya chini anakipata wapi?, hata madiwani wake ambao ndio wawakilishi wa wananchi na wenye kuunda baraza la madiwani, muda mrefu wamekuwa wakilalamikia kuwa hataki kuwaheshimu hasa pale wanapojenga misimamo yenye maslahi ya wananchi wa Mbinga. 

Hivi karibuni baadhi yao ambao ni wajumbe wa kamati ya mipango na fedha wamefikia hatua ya kugoma na kutoka nje ya vikao, kutokana na mkurugenzi huyo kujenga ubishi na kulazimisha mambo ambayo hayana ukweli, kwa kile kinachoelezwa kuwa anafanya hivyo kwa faida ya matakwa yake binafsi. 

Wanasema wanachukizwa na malumbano yanayoendelea sasa kati ya vigogo hao na watendaji wa chini, ambapo muda mwingi mkurugenzi Ngaga amekuwa akifikiria kupanga safu katika idara husika na kuhamisha wakuu wa idara waliokuwepo awali.

“Mkuu wa wilaya tunatambua ndiye mhimili mkuu wa wilaya katika kumwakilisha Rais, inatushangaza kuona mambo haya yanavyokwenda mrama kila kukicha huku akiyakalia kimya, hivi tunahoji hakuna mambo ya kimaendeleo ambayo yeye na mkurugenzi wake wanapaswa kuyafanya kwa manufaa ya wanambinga?, wanahoji.

Ninachoweza kusema katika hili ni vizuri sasa ufike wakati hakuna sababu ya kuendelea kufumbiana macho tukaze kamba na kujenga misimamo imara, kwa kuendelea kupiga vita tabia hii ambayo dhahiri inaonesha wazi kutupeleka kubaya na ni vyema wahusika, wakachukuliwa hatua za kinidhamu kwa lengo la kukomesha hali hiyo.

Jambo la pili ni kwamba, madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga wanalalamikia juu ya suala la ujenzi wa maabara kwa shule za sekondari za serikali wilayani humo, ambapo wanasema badala ya kufanya ujenzi wa majengo mapya kama alivyoagiza Rais Kikwete, mkuu wa wilaya hiyo kwa kushirikiana na mkurugenzi wake wameamua kugeuza baadhi ya majengo yaliyokuwa yakitumika kusomea watoto na kuyafanyia ukarabati kuwa vyumba vya maabara.

Wanasema wao wanatambua kuwa agizo la serikali lilikuwa ni kujenga majengo mapya ya maabara na sio kufanya hiki kilichofanywa hapa Mbinga, ambapo wameeleza kuwa kutokana na shule nyingi za sekondari wilayani humo kuwa na upungufu wa madarasa ya kusomea watoto, jambo hilo lililofanywa litaleta shida na kufanya watoto wakose mahali pa kusomea.

Utafiti uliofanywa na mtandao huu umebaini kuwa halmashauri ya wilaya ya Mbinga ina jumla ya shule za serikali 38, ambapo robo tatu ya shule hizi badala ya kufanya kazi ya ujenzi wa majengo mapya ya maabara uongozi wa wilaya hiyo umefanya maamuzi ya kuchukua vyumba vya madarasa vilivyopo tokea awali, na kuvikarabati wakivifanya ndio vyumba vya maabara kwa masomo ya sayansi huku idadi ya wanafunzi husika waliokuwa wakitumia kusomea katika vyumba hivyo wakikosa sehemu ya kuendelea na masomo.

Kufuatia hali hiyo wanafunzi wamekuwa wakilazimika kulundikana katika majengo machache yaliyopo, huku wazazi wakisema wanahofia uwingi wa watoto waliomaliza elimu ya msingi mwaka huu, ambao wamefaulu kwenda kuanza kidato cha kwanza mwakani katika shule hizo wakisema hilo ni tatizo ambalo litaleta adha kubwa, hivyo ni vyema njia mbadala ikatafutwa haraka ili kunusuru hali hiyo.

Nimezungumza na baadhi ya wananchi na wanafunzi mashuleni kwa nyakati tofauti ambao waliomba majina yao yasitajwe, wanasema wao wanachotambua baada ya serikali kutoa agizo hilo la ujenzi wa vyumba vya maabara, mkuu wa wilaya na mkurugenzi wake wangefanya utaratibu wa kuhamasisha wananchi kuchangia nguvu zao kama ilivyofanyika kwa ujenzi wa shule hizo, na sio kufikia hatua ya kukarabati majengo yaliyopo.

Wanasema katika kuandaa taarifa zao wasije wakathubutu kumdanganya Rais Kikwete kwamba wamejenga majengo mapya ya maabara, wakati shule nyingi wametumia mtindo wa kukarabati madarasa waliyokuwa wakisomea wanafunzi, na kugeuza kuwa chumba cha maabara jambo ambalo linapingana na agizo la serikali la ujenzi wa majengo mapya.

Jitihada ya kumpata mkuu wa wilaya ya Mbinga aweze kuzungumzia juu ya malalamiko haya, hakuweza kupatikana ofisini kwake huku simu yake ikiita kwa muda mrefu bila kupokelewa, na kwamba hata mkurugenzi wake alipokuwa ametembelewa na waandishi wa habari alikuwa akisema “nenda kaandikeni tu”, huku akikataa kutoa ufafanuzi wowote juu ya malalamiko hayo ambayo yapo bado mbele yake.

Binafsi nasema, fikra za hayati Mwalimu Julius  Nyerere na ndoto zake za maendeleo ya Watanzania aliyotaka kuijenga tumeziweka kapuni, viongozi wetu badala ya kujenga daraja wanajitahidi kujenga ukuta ambao unatenganisha fikra za mwalimu na kizazi hiki kipya.

Miaka 25 ya urais wake, sote tunatambua Nyerere aliacha misingi ya utawala bora kwa kila kitu, hivyo kiongozi kufikia mahali kuendekeza migogoro kazini na kuacha kutimiza au kugeuza kinyume maagizo ya kimaendeleo unayopewa na kiongozi wako wa ngazi ya juu, ni sawa na kuleta hasara isiyokuwa na maslahi kwa umma na ukibainika kufanya hivi ni vyema vyombo husika vichukue mkondo wake wa kukuwajibisha ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo.


No comments: