Saturday, December 6, 2014

AFARIKI DUNIA BAADA YA PIKIPIKI ALIYOKUWA AKIENDESHA KUGONGA POWER TILLER



Na Mwandishi wetu,

Tunduru.

STAMILI Mohamed (42) ambaye ni mkazi wa kijiji cha Namiungo wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, amekutwa na mauti baada ya pikipiki aliyokuwa akiiendesha kupata nayo ajali, akiwa katika mwendo kasi.

Taarifa zinaeleza kuwa pikipiki hiyo aliyopata nayo ajali, ni aina ya SUNLG yenye namba za usajili T 339 na kwamba ajali hiyo, ilitokana pia na kuligonga trekta dogo ambalo hutumika kufanyia shughuli za kilimo shambani (Power tiller) na kusababisha kifo chake papo hapo.

Kamanda wa polisi wa mkoa wa Ruvuma  Mihayo Msikhela amethibitisha kuwepo kwa tukio hilo, akieleza kwamba ajali hiyo ilitokea Disemba 4 mwaka huu majira ya usiku.


Awali alieleza kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi aliokuwa nao mwendesha pikipiki huyo, marehemu Mohamed hali ambayo ilimfanya ashindwe kukwepa Power tiller hilo lililokuwa mbele yake.

Mganga aliyeufanyia uchunguzi mwili wa marehemu huyo, Dokta Joseph Ng’ombo alisema kuwa kifo hicho kilisababishwa na kuvuja kwa damu nyingi ndani kwa ndani, kulikosababishwa na  marehemu kujigonga katika bodi trekta hilo.

Dokta Ng’ombo alisema katika ajali hiyo marehemu alipata mivunjiko katika mifupa na mbavu zilizoshikilia kifua, pamoja na kuvunjika mguu wa kushoto mara mbili hali ambayo ilisababisha kutokwa na damu nyingi.

No comments: