Saturday, December 13, 2014

MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA MBINGA, KWA HAYA UNAYOYAFANYA NINGEKUWA MIMI NIMEKUWEKA MADARAKANI NINGEKUFUKUZA KAZI MAPEMA ASUBUHI

Rais Jakaya Kikwete, wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

SIRI juu ya mipango ambayo inaendelea kusukwa chini kwa chini, katika kuhakikisha kwamba Afisa elimu msingi wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Mathias Mkali anachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kufikishwa Mahakamani, kufuatia mgogoro uliotengenezwa na Mkurugenzi wake wa Halmashauri ya wilaya hiyo Hussein Ngaga, zimeanza kuvuja ambapo mtandao huu umeelezwa.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka vyanzo mbalimbali vya habari vimeeleza na kudai kwamba licha ya kuwepo kwa mipango ya kufikishwa Mahakamani Afisa elimu huyo, huenda kama itashindikana katika hilo atachukuliwa hata hatua ya kuhamishwa, ilimradi adhma ya mkurugenzi huyo iweze kutimia kama alivyopanga.

Serikali licha ya kuunda tume na kuja kuchunguza tatizo hili linaloendelea sasa kukera wananchi wa Mbinga, imeonekana tume hiyo kumezwa na vigogo wa halmashauri hiyo wakitaka ilinde maslahi yao binafsi, ikiwemo hudaiwa kushiriki kwa namna moja au nyingine katika kupanga mipango hiyo.

Utafiti uliofanywa na mwandishi wa habari hizi umebaini kuwa, kumekuwa na vikao ambavyo vimekuwa vikifanyika mara kwa mara katika Ikulu ndogo ya Rais wilayani hapa, kati ya vigogo wa wilaya hiyo na wajumbe husika wa tume hiyo hasa nyakati za usiku na mapema alfajiri.


Wadau wa elimu mjini hapa wamekuwa wakihoji, inakuwaje jambo hili la wao kuendelea kukaa katika Ikulu hiyo na kufanya vikao kwa majira hayo jambo ambalo linatia shaka, wakidai kuwa huenda kuna mipango michafu ambayo inaendelea kusukwa chini kwa chini kwa lengo la kulinda maslahi yao binafsi.

Kadhalika kufuatia hali hiyo, baadhi ya wakazi wa wilaya ya Mbinga wameeleza kuwa ni vyema serikali ikachukua hatua ya kufanya mabadiliko ya uongozi wilayani humo, ikiwemo hata kumhamisha mkurugenzi mtendaji au kumchukulia hatua nyingine za kinidhamu ili kuweza kunusuru migogoro ya hapa na pale isiweze kuendelea, ambayo yeye ndiye kinara wa kuitengeneza na kutishia ustawi wa maendeleo wilayani hapa. 

Mkurugenzi Ngaga anakuza mgogoro huo ambao umejenga hata nyufa na kutengeneza makundi kwa baadhi ya watendaji wa serikali na madiwani, kufuatia kwa kile kinachoelezwa kuwa amekuwa mwiba kwa afisa elimu huyo, kutokana na Mkali kuwa na misimamo yake ya kazi hususani katika kusimamia fedha na maendeleo ya elimu msingi wilayani humo.

Ngaga analalamikiwa akidaiwa kufanya mchezo mchafu wa kuchota fedha za maendeleo ya idara hiyo ya elimu, ambapo hata sasa walimu wengi wa wilaya hiyo wamekuwa wakilalamika kutolipwa madai yao ya msingi ikiwemo fedha za uhamisho na malimbikizo ya likizo.  

Hata hivyo hivi karibuni shilingi milioni 54,725,000 kutoka katika mfuko wa fedha za ruzuku kwa ajili ya kuendeshea mitihani mashuleni (Capitation) Mkurugenzi huyo alichota fedha hizo, kwa madai kuwa anaziazima na kwamba atazirejesha lakini baada ya Afisa elimu Bw. Mkali kwenda kumtaka azirudishe ndipo alionekana kuwa mbogo huku akiwa mkali na kumfokea.

Taarifa zilizotufikia na kuthibitishwa na vyanzo mbalimbali vya habari kutoka ndani ya halmashauri ya wilaya ya Mbinga, vimesema kuwa hata hivyo baada ya fedha hizo kuonekana zinamletea shida huku akihofia kujibu hoja za ukaguzi na kukwepa matatizo yanayoweza kujitokeza baadaye, aliamua kuchukua jukumu la kuzirejesha haraka kwenye akaunti husika licha ya kukaa nazo muda mrefu, na wanafunzi mashuleni wakikosa huduma za msingi.

No comments: