Friday, December 19, 2014

WAANDIKISHAJI NA WASIMAMIZI UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA WILAYANI MBINGA WALALAMIKIA POSHO ZAO

Waziri wa TAMISEMI Hawa Ghasia (kulia) pamoja na Katibu mkuu TAMISEMI Jumanne Sagini. (kushoto)
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

KASORO za uchaguzi zilizojitokeza katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika hivi karibuni hapa nchini, pia hali ya hewa imechafuka wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma kufuatia baadhi ya Waandikishaji na Wasimamizi wa uchaguzi huo, kumlalamikia Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo Hussein Ngaga, kwamba malipo ya posho walizolipwa katika zoezi hilo amewalipa kidogo, tofauti na maeneo mengine nje ya wilaya hiyo.
Aidha kufuatia hali hiyo Waandikishaji na Wasimamizi hao wamemuomba Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Hawa Ghasia, kuingilia kati na kuweza kulifanyia kazi jambo hilo ili waweze kupata haki yao ya msingi kwa kazi waliyofanya.
Malalamiko hayo yalitolewa kwa nyakati tofauti walipokuwa wakizungumza na mwandishi wa habari hizi, kwa kuomba majina yao yasitajwe gazetini ambapo walisema kuwa hata wakati wanafanyiwa semina na kupewa miongozo juu ya utekelezaji wa zoezi hilo, hawakulipwa posho badala yake waliambiwa kwamba watalipwa mara baada ya uchaguzi kufanyika.

Kwa mujibu wa mtoa habari wetu alidai kuwa siku ya mwisho ya uchaguzi huo wamesainishwa fomu ya malipo shilingi 85,000 lakini cha kushangaza fedha taslimu waliyokabidhiwa mkononi ni shilingi 50,000 tu, jambo ambalo walipojaribu kuhoji hakuna majibu sahihi waliyopewa.
Waliendelea kudai kuwa maeneo mengine wilayani humo, waandikishaji wamelipwa shilingi 35,000 kwa siku saba, ambapo kwa siku moja walikuwa wakilipwa shilingi 5,000 jambo ambalo wamekuwa wakilalamika kuwa ni kidogo, tofauti na maeneo mengine nje ya wilaya hiyo wenzao walikuwa wakilipwa shilingi 10,000 hadi 15,000 kwa siku wakati wanafanya zoezi hilo la uandikishaji wapiga kura.
“Sisi tunasikitishwa na malipo haya kidogo, hata wakati tunafanyiwa semina juu ya zoezi hili hatukulipwa kitu tulikuwa tunatumia fedha zetu wenyewe za mifukoni, Mkurugenzi mtendaji alituma taarifa kwetu wakati tunafanyishwa semina kwamba halmashauri haina fedha zimetumika kwenye mambo ya ukaguzi tumvumilie atatulipa siku ya mwisho ya uchaguzi na ndivyo alivyofanya”, walisema.
Jitihada ya kumpata Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga Bw. Ngaga ofisini kwake, ili aweze kutolea ufafanuzi juu ya malalamiko hayo hazikufanikiwa na simu yake ya kiganjani ilikuwa haipatikani.

No comments: