Saturday, December 13, 2014

TUME YATILIWA MASHAKA, BAADHI YA VIGOGO MBINGA WADAIWA KUTENGENEZA MBINU CHAFU KUHARIBU UKWELI ULIOPO

Waziri Mkuu Mizengo Pinda.
Na Mwandishi wetu,
Mbinga.

TUME ya watu wawili ambayo imeundwa na serikali, kwa ajili ya kuja kuchunguza mgogoro uliopo kati ya Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Hussein Ngaga na Afisa elimu msingi wa wilaya hiyo, Mathias Mkali imetiliwa shaka huku ikinyoshewa kidole na kudaiwa kutotenda haki kutokana na tume hiyo kuonekana ikiegemea upande wa mkurugenzi huyo.

Baadhi ya wadau wa elimu wakiwemo na watendaji wa serikali, ambao wameteuliwa kwa ajili ya kuhojiwa walisema hayo mjini hapa, wakati walipokuwa wakizungumza kwa nyakati tofauti na mwandishi wetu mara baada ya kufanyiwa mahojiano na tume hiyo.

“Mambo tunayoulizwa ndani ya tume mengi yanaonesha ni yale yale ambayo yametengenezwa na mkurugenzi, sisi tunapotaka kutoa hoja zetu za msingi tunabanwa sana na kunyimwa uhuru wa kujieleza kweli hapa kuna haki? au tume hii imekuja kwa ajili ya kumbeba mtu”, ? walihoji.

Walisema wanashangazwa kuona wakati mwingine tume imekuwa ikihoji kwa kutumia lugha za vitisho, zenye kuonyesha kubeba kundi la upande mmoja na kwamba chumba cha mahojiano kilichopo katika jengo la ukumbi mdogo wa halmashauri ya wilaya hiyo, wahojiwa wamekuwa hawapewi uhuru wa kutosha wakati wa kujieleza jambo ambalo linajenga kukosa imani nao.

Aidha walieleza kuwa wanashangazwa kumuona Afisa utumishi wa wilaya ya Mbinga, Emmanuel Kapinga, kuwepo ndani ya chumba cha mahojiano na tume hiyo ambapo wakati wa mahojiano muda mwingi amekuwa mtu wa kupinga na kuwa mkali pale mhojiwa anapokuwa akitoa maelezo yenye ukweli juu ya jambo husika linaloulizwa kutoka kwa mjumbe wa tume.


Watu wengi wamekuwa wakihoji, kama tume hiyo imepewa uhuru wa kufanya kazi si jambo la busara kwa afisa utumishi huyo Bw. Kapinga, kuwepo katika chumba cha mahojiano na kupinga maelezo yenye ukweli ambayo yanatolewa na wahojiwa hivyo hali hiyo endapo itaendelea, hapo hakuna uhuru wa tume katika kutenda haki juu ya mgogoro huu ambao unaendelea kufukuta hadi sasa.

Hali hiyo walifafanua kuwa ni kunyima uhuru wa wahojiwa namna ya kujieleza kwa yale mambo muhimu waliyonayo, hivyo kuna kila sababu ya tume hiyo kutiliwa mashaka kutokana  na mwenendo huo unaoendelea sasa.

Pia Uchunguzi uliofanywa na mtandao huo umebaini kuwa, tume hiyo hata sehemu ya malazi wameandaliwa na vigogo wa wilaya hiyo ambapo baadhi ya wananchi wamekuwa wakihoji kwamba, kitendo hicho kinaashiria kuwepo kwa mianya ya rushwa ambayo itapelekea haki kutotendeka.

Ikulu ndogo ya Rais iliyopo wilayani hapa, ndiyo sehemu ambayo tume hiyo imeweka kambi kwa ajili ya malazi na kwamba nimeshuhudia kumekuwa na mfululizo wa magari ya baadhi ya vigogo wa ngazi ya juu wa wilaya ya Mbinga  hasa majira ya usiku na mapema alfajiri, wamekuwa wakienda huko kuzungumza nao jambo ambalo ni dalili tosha kwamba kuna mbinu chafu ambazo zinaendelea kusukwa kwa lengo la kuvuruga ukweli wa jambo ambalo linachunguzwa.

Mkuu wa wilaya hiyo Senyi Ngaga, Mkurugenzi mtendaji Hussein Ngaga, Katibu tawala Stephano Ndaki na Afisa usalama wa Taifa wa wilaya (Jina tunalo) ndio ambao wamekuwa mara kwa mara wakionekana kwenda katika Ikulu hiyo, ambako tume hiyo imeandaliwa malazi.

Wadau wa elimu wanasema ni vyema tume hiyo ingeachwa huru wakati inapofanya kazi zake bila kuingiliwa na mtu yeyote, ili mwisho wa siku jamii iweze kupata ukweli juu ya mgogoro huu uliopo kati ya mkurugenzi huyo na afisa elimu wake.

Mwenyekiti wa tume hiyo, Philemon Bossy alipozungumza na waandishi wa habari juu ya tuhuma hizo zinazoelekezwa kwa tume hiyo anayoiongoza, alikana kuwepo kwa mambo hayo na kusema kuwa wao wamekuja kufanya kazi ya kuchunguza tuhuma zilizopo.

“Sisi tunapowahoji wahusika ni lazima afisa utumishi naye awepo ndani ya tume, yeye anakuwa kama shahidi wakati mahojiano yanayoendelea kufanyika kwa sababu tumekuja kuchunguza mambo ya kiutumishi, hivyo si makosa kwa yeye kuwepo wakati tunapohoji”, alisema.

Hata hivyo Philemon aliongeza kuwa hata Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga, Hussein Ngaga naye alikuwa akilazimisha awepo ndani ya chumba cha mahojiano lakini alimkatalia na kumwambia kuwa hatakiwi kuwepo na endapo kama litafanyika hilo, itakuwa ni tendo la uvunjifu wa taratibu na sheria husika.

No comments: