Saturday, May 14, 2016

FEDHA ZA UCHAGUZI SHILINGI MILIONI 513 ZADAIWA KUTAFUNWA MKUU WA WILAYA MBINGA AWAJIA JUU WATENDAJI WAKE WA HALMASHAURI


Na Kassian Nyandindi,

Mbinga.

MKUU wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Senyi Ngaga amewajia juu watendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo ambao wanadaiwa kuhusika kwa namna moja au nyingine kufanya ubadhirifu wa fedha shilingi bilioni 1.4 ambazo zilitolewa na serikali kwenda wilayani humo, kupitia Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa ajili ya kufanya kazi iliyolengwa katika uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25 mwaka jana.

Ngaga alisema kuwa ubadhirifu huo umebainika, baada ya ofisi yake kuunda tume ndogo ambayo ilifanya kazi kwa ushirikiano wa baraza la kamati ya ulinzi na usalama la wilaya hiyo na kuweza kubaini wizi huo, uliofanyika katika fedha hizo za serikali.

Senyi Ngaga, Mkuu wa wilaya ya Mbinga.
Aidha alisema kuwa tume hiyo iliyoundwa ambayo inaendelea na uchunguzi wake na majina ya waliohusika kuwekwa bayana hapo itakapomaliza kazi yake, ambapo taarifa za awali katika fedha hizo zinathibitisha kwamba maofisa waliopewa dhamana ya kuendesha uchaguzi huo wilayani hapa kwa kushirikiana na idara ya fedha na manunuzi ya wilaya hiyo, ndio wanaodaiwa kuhusika kutengeneza mianya ya kutafuna fedha hizo.

Hayo yalisemwa na Mkuu wa wilaya hiyo, Ngaga kwenye kikao cha baraza la Madiwani wilayani humo kilichoketi juzi kwenye ukumbi wa Umati uliopo mjini hapa na kwamba alieleza kuwa ubadhirifu huo umefanyika kupitia watu kulipana posho, ununuaji wa mafuta na vipuri vya magari, chakula na vifaa vingine vya ofisi (Stationary) kinyume na taratibu za miongozo iliyotolewa na serikali.


Mkuu huyo wa wilaya alifafanua kuwa mpaka sasa kati ya fedha hizo zilizotolewa na NEC wameweza kubaini ubadhirifu wa shilingi milioni 513 ambazo hazikufuata taratibu na miongozo husika katika matumizi yake, ambapo kati ya hizo shilingi milioni 822 zimetumika watu kulipana posho, shilingi milioni 140 kwa ajili ya kusambaza vifaa vya maofisini, shilingi 135 zimetumika kununua vipuri vya magari na mafuta na kwamba shilingi milioni 85 zimetumika kwa ajili ya chakula.

Akielezea juu ya fedha zilizotumika kununulia vifaa vya ofisi shilingi milioni 140, alisema kuwa tume hiyo aliyoiunda kuchunguza matumizi ya fedha hizo imebaini kuwa fedha zilizotumika kununulia vifaa hivyo ni shilingi milioni 4 tu na sio zaidi ya fedha hizo, ambapo suala hilo lilithibitishwa baada ya tume kumhoji mzabuni husika ambaye alipewa kazi ya kusambaza vifaa hivyo vya ofisini.

Vilevile alieleza kuwa fedha zilizotumika kununulia vipuri vya magari shilingi milioni 135 mzabuni aliyetumika kufanya kazi hiyo, hana duka au kampuni ambayo ingeweza kumfanya aweze kuwa na sifa katika mchakato wa manunuzi ya vifaa husika jambo ambalo linaleta mashaka na kujenga mianya ya wizi wa fedha za umma.

“Mheshimiwa Mwenyekiti hali hii inasikitisha sana, hata mafuta yaliyonunuliwa kwa ajili ya kufanikisha zoezi la uchaguzi mkuu cha kushangaza katika taarifa za fedha baada ya tume yangu kuchunguza, imegundua kwamba mafuta mengine yalitumika kujaza kwenye katapila la halmashauri, malori ya kubeba mizigo na pikipiki wakati huo wahusika waliopewa dhamana ya kusimamia jambo hili wakijua kwamba hayahusiki kwenye shughuli za uchaguzi”, alisema Ngaga.

Ngaga aliongeza kuwa ameshangazwa na ofisi ya Mkaguzi wa ndani wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga, kutofanyia kazi jambo hilo na kutolea taarifa katika vikao vya baraza la madiwani huku akiagiza na kumtaka mkaguzi huyo wa ndani wilayani humo, kuhakikisha kwamba kuanzia sasa anafanya kazi zake kwa uwazi na sio kuficha ukweli wa ubadhirifu wa fedha ambao hufanywa na watumishi wasio kuwa waaminifu katika halmashauri hiyo.

“Kwa nini nimesema hivyo, ndugu zangu nimesema hivyo ili madiwani muweze kuelewa vyombo vya dola vinaendelea na kazi yake hatutaishia hapa jambo hili tutalifikisha mpaka ngazi ya juu na wale waliohusika kufanya ubadhirifu huu watavuna walichopanda sipendi kumuonea mtu, watumishi wa serikali fanyeni kazi kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa tuache kufanya kazi kwa mazoea”, alisisitiza.

Kufuatia hali hiyo, kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga, Ambrose Mtarazaki alimuagiza kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Samwel Komba kuhakikisha kwamba suala hilo anajenga ushirikiano wa karibu na ofisi ya Mkuu wa wilaya hiyo, ili liweze kufanyiwa kazi haraka na wahusika waliofanya ubadhirifu huo wachukuliwe hatua kwa mujibu wa taratibu na sheria za nchi ili iweze kuwa fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo.

No comments: