Wednesday, May 4, 2016

GAMA AFANYA UZINDUZI WA JIMBO CUP

Leonidas Gama, Mbunge wa Songea mjini.
Na Julius Konala,
Songea.

MBUNGE wa jimbo la Songea mjini mkoani Ruvuma, Leonidas Gama amefanya uzinduzi wa tamasha la michezo lijulikanalo kwa jina la Jimbo Cup, ambalo litashirikisha kata 21 za Manispaa ya Songea mkoani humo.

Uzinduzi huo ulifanyika hivi karibuni kwenye uwanja wa michezo Majimaji uliopo mjini hapa, ambapo mamia ya wananchi wa Manispaa hiyo waliweza kushiriki ikiwemo na vikundi mbalimbali vya sanaa.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Gama alisema lengo la kuandaa tamasha hilo ni kwa ajili ya kuimarisha tamaduni za mkoa wa Ruvuma, ikiwemo hata kuibua na kukuza vipaji vya vijana.


Vilevile alieleza kuwa kupitia tamasha hilo, wataweza kuimarisha afya zao na kuufanya mji wa Songea kuwa wa michezo pamoja na kuutangaza vivutio vyake vya utalii.

Mbunge huyo alisema sababu kubwa ya kufanya tamasha hilo ni kuweza pia kuufanya mji huo, kuwa kisima cha kuzalisha wasanii na wachezaji mbalimbali wa mpira wa miguu ili timu ya Majimaji iweze kupata wachezaji wenye vipaji.

Amewataka wananchi wa Manispaa hiyo, kujenga ushirikiano katika kufanikisha jambo hilo kwa lengo la kuleta mabadiliko chanya.

Kadhalika Gama ameyaomba makampuni mbalimbali, kujitokeza katika kudhamini mashindano hayo ambayo yanaendelea kufanyika mjini hapa na kilele chake kitakuwa Mei 7 mwaka huu.

Katika uzinduzi wa tamasha hilo, michezo mbalimbali ilichezwa ikiwemo kutembea mita 800 kuzunguka uwanja, kuvuta kamba, kufukuza kuku, miziki ya kizazi kipya ilipigwa, ngoma za utamaduni na mpira wa kengele ambao ulichezwa na walemavu wa macho (wasioona).

No comments: