Friday, May 13, 2016

WATUMISHI HEWA MBINGA WAJISALIMISHA POLISI WALIPA FEDHA ZA SERIKALI WALIZOJIPATIA ISIVYO HALALI


Na Kassian Nyandindi,

Mbinga.

ZOEZI la uhakiki Watumishi hewa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, linaendelea kupamba moto ambapo watumishi 46 ambao walikwisha staafu wamebainika kuendelea kuchukua mishahara hewa, huku wakijua kwamba kufanya hivyo ni kinyume cha sheria na taratibu za nchi.

Rais John Pombe Magufuli.
Aidha kufuatia msako mkali unaoendelea kufanyika na timu ya uongozi wa halmashauri hiyo, kati ya hao watumishi 14 wamejisalimisha kituo kikuu cha Polisi wilayani humo na kwamba wamewekwa mahabusu, kutokana na kujipatia fedha hizo isivyo halali.

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga, Venance Mwamengo alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake na kuongeza kuwa asilimia kubwa ya waliokamatwa ni wa kutoka idara ya kilimo na elimu.


Alifafanua kuwa watumishi 24 wameanza kurejesha fedha walizochukua ambapo hadi kufikia Aprili 28 mwaka huu, jumla ya shilingi milioni 31 zimekusanywa na kurejeshwa hazina.

“Lengo letu ni kuhakikisha kwamba watumishi wote hewa wanabainika na kuchukuliwa hatua za kisheria, ikiwemo wote hawa tuliowakamata na tutakaoendelea kuwakamata watafikishwa Mahakamani ili fedha hizi za wananchi ziweze kupatikana na kurejeshwa sehemu husika”, alisema Mwamengo.

Alibainisha kuwa uhakiki wa awali waliweza kuwakamata watumishi hewa 22 na kadiri ya zoezi hilo linavyoendelea kutekelezwa, walipatikana wengine 24 na kwamba uhakiki huo bado unaendelea.

Pia Mkurugenzi huyo alitoa rai kwa watumishi ambao wanajua kwamba wamestaafu na bado wanaendelea kuchukua mishahara kila mwezi, wairejeshe mapema kabla mkono wa sheria haujawafikia.

Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Ruvuma, Zubery Mwombeji amethibitisha kukamatwa kwa watumishi hao na wengine wakijisalimisha wenyewe kurejesha fedha za serikali, ambazo walikuwa wakijipatia kwa njia isiyokuwa halali.

Hata hivyo Mwombeji alieleza kuwa, kwa wale ambao walikamatwa na kuwekwa mahabusu wapo nje ya dhamana wakati taratibu za kuwafikisha mahakamani zikiendelea kufanyika.

No comments: