Saturday, May 14, 2016

AFARIKI DUNIA KWA KUVILIGWA NA WAYA WA UMEME



Na Steven Augustino,
Tunduru.

WATU wawili wamefariki dunia katika matukio tofauti, yaliyotokea wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, likiwemo la mtu mmoja kuviligwa na waya wa umeme wakati akipita barabarani.

Zubery Mwombeji.
Taarifa za matukio hayo zinasema kuwa tukio la kwanza lilitokea katika msitu wa hifadhi ya Muhuwesi, baada ya mkazi wa kitongoji cha Ngoloanga kijiji cha Chalinze Kata ya Muhuwesi, Fakii Rashid Mabula (43) alikutwa akiwa amefariki dunia baada ya kung'atwa na nyoka.

Mwenyekiti wa kitongoji hicho, Said Omari Likomanje alisema kuwa mwili wa marehemu huyo uligundulika Mei 5 mwaka huu baada ya kuripotiwa kupotea tangu Mei 1 mwaka huu, kwa madai kuwa alikwenda katika msitu huo kwa ajili ya kutafuta mabanzi ya kujengea zizi lake la mifugo.


Alisema katika tukio hilo mashuhuda hao, walibaini kwamba marehemu aliumwa na nyoka baada ya kuona kamba ambazo alikuwa amejifunga katika maeneo mawili ya mguu wake pamoja na meno ya nyoka huyo, jambo lililowafanya wabaini kuwa kifo chake kilisababishwa na kuzidiwa na sumu ya nyoka huyo.

Kwa mujibu wa taarifa za tukio la pili, ambalo lilitokea katika eneo la nguzo sita, katika bara bara ya Tunduru kuelekea Songea ambapo mtu aliyefahamika kwa jina la Yusufu Niiya (32) alifariki dunia baada ya kuviligwa na waya wa umeme.

Mashuhuda wa tuio hilo walisema kuwa marehemu huyo, alikuwa anatoka katika eneo la Mwembeliziki kwenda nyumbani kwake eneo la kijiji cha Nakayaya wilayani humo.

Walisema wakati akiwa njiani, ghafla Lori la mafuta ambalo lilikuwa likipita bara barani liligonga nguzo na kukata nyaya hizo ambazo zilimuangukia na kusababisha marehemu kunaswa na umeme, huku dereva aliyekuwa akiliendesha alilitorosha kwa lengo la kukimbia ili asiweze kupatikana katika eneo hilo la tukio.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma, Zubery Mwombeji amethibitisha kuwepo kwa taarifa hizo na kwamba bado wanaendelea na uchunguzi wa matukio hayo.

Mwombeji ametoa mwito kwa wananchi wenye taarifa za kujitosheleza juu ya matukio hayo, walisaidie jeshi hilo kuwanasa mapema watuhumiwa wa matukio hayo ili waweze kufikishwa kwenye vyombo vya kisheria.

No comments: