Sunday, May 22, 2016

AFISA ARDHI TUNDURU AHUKUMIWA KWENDA JELA MIAKA MIWILI



Na Steven Augustino,
Tunduru.

MAHAKAMA ya wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, imemhukumu Ofisa mthamini ardhi mstaafu wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Bernad Nyasi (60) kutumikia kifungo cha miaka miwili jela baada ya kupatikana na hatia katika kosa la kughushi nyaraka na kutoa hati za uongo, kwa wateja waliotakiwa kupewa vipande vya ardhi wilayani humo.

Adhabu hiyo ambayo pia ilimpatia nafasi kwa kumtaka mtuhumiwa huyo kulipa faini ya shilingi 500,000 ilitolewa na Hakimu mfawidhi wa Mahakama ya wilaya hiyo, Gladys Barthy baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa katika shauri hilo la jinai namba 6/2016.

Katika hukumu hiyo Mahakama hiyo, pia imewaachilia huru washtakiwa wengine wawili waliokuwa wanakabiliwa na shtaka hilo ambapo  mpima ardhi wa Halmashauri hiyo, Mohamed Hamis (35) na mhudumu wa ofisi ya ardhi ya wilaya ya Tunduru Masud Kanduru (40).

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka hayo, Mahakama hiyo ilimkuta na hatia Ofisa ardhi huyo katika shtaka la nane kati ya makosa 10 yaliyokuwa yanawakabili watuhumiwa hao ambalo ni la kughushi hati namba TUR/77 ya Mei 20 mwaka 2015 iliyokuwa ikimtambulisha Mariam Nyenje kuwa ni mmiliki halali wa kiwanja namba 104 Ploti namba 0 katika eneo la Nakayaya wilayani hapa.


Akiwasomea mashitaka hayo Mwendesha mashtaka mkaguzi msaidizi wa Polisi Inspekta Songelael Jwagu, alisema kuwa pamoja kwamba watuhumiwa hao walifanya kosa la kughushi nyaraka mbalimbali kinyume cha sheria namba 333 na 335 (a) na 337 vya sheria ya kanuni ya adhabu sura namba 16, kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Katika mashtaka hayo pia watuhumiwa hao, walidaiwa kutenda kosa la kuwasilisha hati za uongo kwa wateja wao kinyume cha sheria namba 342 cha kanuni ya adhabu sura ya 16.

Inspekta Jwagu alisema mnamo Julai Mosi mwaka 2013 watuhumiwa hao walighushi barua yenye kumbukumbu namba TUR/ 7914 ikiwa inamtaja Maembe Sabule Wambura, kuwa ndiyo mmiliki halali wa kiwanja namba 152, kitalu FF kilichopo katika mtaa wa Nakayaya mjini hapa.

Aliwataja wengine ambao walitapeliwa kwa mtindo huo kuwa ni, Rashid Athuman Issa aliyeandikiwa hati namba TUR/8811/Q ya Disemba 7 mwaka 2014 ikiwa inamtambulisha kuwa yeye ndiye mmiliki halali wa kiwanja namba 190, kitalu namba Q kilichopo katika eneo hilo la Nakayaya.

Pia katika hati hiyo alilitaja shtaka jingine, lililokuwa linawakabili watuhumiwa  hao kuwa ni shauri la kughushi barua yenye kumbukumbu namba Tu/9080 /1/BSR ya Julai 1 mwaka 2013 ikiwa inaonesha kwamba iliandikwa na Ofisa ardhi wa wilaya hiyo, Nyasi ikimpatia idhini Peter Rioba Mnanka kuwa ndiyo mmiliki halali wa kiwanja namba 53 kitalu 0 kilichopo kwenye eneo la Nakayaya Tunduru mjini.

No comments: