Tuesday, May 24, 2016

WANANCHI WAISHIO PEMBEZONI MWA TUNDURU WATESEKA NA MAMBA MTO RUVUMA



Na Steven Augustino,
Tunduru.

WATU watatu wamelazwa katika hospitali ya Misheni ya Mbesa wilayani Tunduru mkoani Ruvuma, baada ya kujeruhiwa na mamba katika matukio tofauti yaliyojitokeza wilayani humo.

Hayo yamebainishwa na Mganga mkuu wa hospitali hiyo, Dokta Ires Sekreman wakati alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu katika mahojiano yaliyofanyika kwa njia ya simu, ambapo pamoja na mambo mengine hospitali hiyo ambayo ipo pembezoni mwa Tanzania imekuwa msaada mkubwa kwa wananchi hao, ambao hukumbwa na matatizo ya aina mbalimbali ya kiafya.

Dokta Sekreman alisema kwamba amekuwa akipokea majeruhi na wagonjwa wengi kutoka katika vijiji vilivyopo nchi jirani ya Msumbiji hasa ambao hujeruhiwa na mamba, ambayo huwapata wakati wakivua samaki na kufanya shughuli hizo katika mto Ruvuma.


Alimtaja majeruhi wa kwanza kuwa ni, Addo Adam (29) mkazi wa kijiji cha Kazamoyo tarafa ya Lukumbule wilayani Tunduru ambapo kutokana na hali aliyokuwa nayo majeruhi huyo, maafisa tabibu na wataalamu wa hospitali hiyo ya Mbesa walikubaliana kumkata mguu wake  wa kulia ili kuokoa maisha yake kutokana na kuharibiwa vibaya.

Alisema majeruhi huyo ambaye alipokelewa April 16 mwaka huu, mguu huo uliharibika vibaya baada ya kutafunwa na mamba huyo na kwamba endapo kama usingekatwa ungeoza na kumfanya apoteze maisha.

Kadhalika alimtaja majeruhi mwingine kuwa ni Sharif Makunga ambaye pia alikuwa akipatiwa huduma ya matibabu katika hospitali hiyo, kutokana na kujeruhiwa na mamba.

Akizungumzia matukio hayo kaimu Afisa wanyamapori wilayani Tunduru, Peter Mtani pamoja na kuthibitisha uwepo wa matukio hayo alifafanua kuwa katika kipindi hicho, Zainabu Kopwe aliuawa na mamba katika mto huo wakati akiwa anaoga ambapo tukio hilo lilitokea March 18 mwaka huu.

Mtani alisema kuwa chanzo cha matukio hayo, kinatokana na jamii wakati wote katika uwanda huo wa mto Ruvuma hutegemea maji ya mto huo kwa shughuli mbalimbali.

Alisema katika matukio yote  yaliyoripotiwa na ambayo mengine idara yake haikuyapata huwatokea hasa wakiwa wanaoga, kuchota maji kwa ajili ya kunywa na kufulia nguo zao, huku wengine hupatwa na mikasa hiyo pale wanapokwenda kuvua samaki kwenye mto huo.

Hata hivyo alisema suluhisho kubwa namna ya kuwaepusha watu hao ili waweze kuepukana na matatizo hayo, kuna kila sababu kwa serikali kufanya jitihada ya kuwapelekea maji safi na salama ya bomba au kisima, ili waweze kuepukana na kadhia hiyo wanayoendelea kuteseka nayo kwa muda mrefu sasa.

No comments: