Monday, May 23, 2016

UKWELI JUU YA UBADHIRIFU FEDHA ZA UCHAGUZI MKUU MBINGA UPO WAPI?


Na Kassian Nyandindi,

SERIKALI siku zote imekuwa ikiwataka watumishi au watendaji wake wa serikali, kufanya kazi kwa uadilifu mkubwa na kuachana na vitendo vya ubadhirifu wa fedha au mali za umma.

Kassian Nyandindi, Mwandishi wa makala haya.
Tuhuma za wizi wa fedha tumekuwa tukizisikia kupitia vyombo vya habari kila kukicha, kufuatia viongozi waliopo madarakani kuibua hoja hizo na kuunda tume za kuchunguza mambo haya ili kuweza kubaini wabadhirifu waliohusika kufanya hivyo.

Katika makala haya ya uchambuzi, napenda kuelezea kwa ufupi juu ya mwenendo wa hoja iliyotolewa hivi karibuni wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, kuhusiana na fedha za Uchaguzi Mkuu uliofanyika mwaka jana zinazodaiwa kufanyiwa ubadhirifu kutokana na ukiukwaji wa matumizi mabaya au kutofuata miongozo husika ya matumizi yake.

Tuhuma za ubadhirifu wa fedha hizo shilingi bilioni 1.4 ambazo zilitolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwenda kwa Halmashauri ya wilaya hiyo kufanya kazi iliyolengwa, ilitolewa na Mkuu wa wilaya hiyo Senyi Ngaga katika baraza la Madiwani wa halmashauri hiyo ambalo liliketi Mei 11 mwaka huu mjini hapa.


Baada ya Ngaga kueleza juu ya wizi huo unaodaiwa kufanywa katika fedha hizo za uchaguzi, ilikuwa ni sawa kazua mgogoro mkubwa unaoendelea kufukuta kila kukicha kati ya ofisi yake na kwa upande wa halmashauri hiyo kufuatia baadhi ya watendaji (majina tunayo) wakidai kwamba suala hilo halina ukweli na kiongozi huyo ambaye anamwakilisha Rais, hawakutegemea atafanya hivyo huku wengine wakisema “amekurupuka kusema kwamba fedha hizo zimefanyiwa ubadhirifu”.

Kila nilipokuwa nikilala na kuamka asubuhi na kuendelea kufanya tafiti juu ya jambo hili kwa kupata hoja za kutoka pande zote, binafsi nimebaini kwamba bado jambo hili limejaa utata mtupu.

Wengine wanahoji kama fedha hizo zingetafunwa je, uchaguzi katika wilaya hiyo ungefanyika kwa ufanisi, huku taarifa zilizotolewa na Mkuu huyo wa wilaya katika kikao hicho kwamba kati ya fedha hizo shilingi milioni 513, ndizo zinazodaiwa kutafunwa.

Lakini katika utafiti wangu nilioufanya takribani wiki moja sasa imepita, pia unathibitisha kuwa zaidi ya shilingi milioni 150 kati ya fedha hizo shilingi bilioni 1.4 baada ya uchaguzi huo kumaliza kufanyika wilayani humo, zilirejeshwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Tunatambua kwamba suala hili limefikishwa kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilayani Mbinga na hata ngazi zingine za juu, kwa lengo la kukamilisha uchunguzi wa kina zaidi na wahusika waliofanya ubadhirifu huo, waweze kuchukuliwa hatua za kisheria na kuwekwa hadharani ili wananchi waweze kuwatambua.

Nasema TAKUKURU ni chombo ambacho kimekuwa kikifanya kazi zake kwa weledi na hatimaye mwisho siku, hatutegemei kuona jambo hili likiendelea kukaa kimya kwa muda mrefu bila wananchi kujua hatma yake, vinginevyo sitakosea nikisema kama lilikuwa bado linafanyiwa utafiti kwa nini lilitangazwa kwenye baraza la Madiwani?.

Binafsi kwa elimu yangu ya taaluma ya habari ambayo nimebobea kwa miaka mingi nikirejea kauli za wataalamu wa masuala ya uchunguzi au tafiti mbalimbali siku zote huwa wanasema; jambo lolote kama linafanyiwa utafiti au uchunguzi na ukweli wake bado haujakamilika sio vyema tuhuma zake kuziweka mapema hadharani, hivyo basi walioliweka hadharani tunatambua wanajua ukweli wake hatuhitaji kuendelea kuwasikia eti uchunguzi bado unafanyika au kukaa kimya kwa muda mrefu, bila kutoa taarifa ya wazi na yenye ukweli juu ya tatizo hili na hatua gani zimechukuliwa. 

Tunataka kujua hatma ya tatizo hili kama ni la kweli au sio kweli, lakini pia kuendelea kuchelea wakati huo lilikwisha ripotiwa wazi mbele ya hadhira yaani kwenye kikao cha baraza la Madiwani ni sawa na kuendelea kujenga maswali mengi miongoni mwetu, hususani kutoka kwa wananchi na ndio maana leo hii wengine hufikia hatua ya kusema “DC kakurupuka kusema kwamba fedha hizo zimefanyiwa ubadhirifu”.

Hatutegemei yaendelee kusemwa maneno haya, bali tunachohitaji hapa ni ukweli na uwazi wa jambo hili na sio kumwonea mtu, siku zote wananchi huwa tunaamini kwamba kinachosemwa na serikali huwa ni cha kweli na kimefanyiwa utafiti wa kina hivyo tunasubiri kuona ni hatua zipi zinachukuliwa, ili wananchi tuendelee kujenga imani na viongozi wetu waliopo madarakani ambao wamepewa dhamana ya kutuongoza hasa tukizingatia kwamba kasi ya utendaji kazi kwa serikali yetu ya awamu ya tano ni nzuri na falsafa yake ya kupendeza ya "hapa kazi tu".

nyandindi2006@yahoo.com au 0762 - 578960

No comments: