Wednesday, May 11, 2016

WAKULIMA WA TUMBAKU WATAKIWA KUTOKATISHWA TAMAA

Na Mwandishi wetu,
Namtumbo.

WAKULIMA wa zao la tumbaku wilayani Namtumbo mkoa wa Ruvuma, wametakiwa kutokatishwa tamaa kutokana na changamoto mbalimbali zinazolikabili zao hilo, badala yake waongeze juhudi katika uzalishaji wake hatua ambayo itawawezesha kuinua  hali zao za maisha.

Wito huo ulitolewa na  Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Alli Mpenye alipokuwa akifafanua juu ya mikakati mbalimbali ya kufufua zao hilo kwa waandishi wa habari, ofisini kwake.

Aidha Mpenye alibainisha kuwa, tatizo la kushuka kwa uzalishaji wa zao la tumbaku  wilayani humo katika miaka ya hivi karibuni kumechangiwa na wakulima kukatishwa tamaa na viongozi wa vyama vya ushirika wilayani humo,  ambao walishirikiana na makampuni yanayonunua tumbaku kuwaibia wakulima na hata wakati mwingine kuwabambikia madeni makubwa ya pembejeo.

Kadhalika ameishukuru serikali kuanza kuwachukulia hatua za kisheria viongozi wote waliohusika kutafuna fedha za wakulima hao, na wale walioua vyama vya ushirika ambao kwa kiasi kikubwa ndiyo walishiriki kwa namna moja au nyingine kuua zao la tumbaku kwa kufanya vitendo visivyofaa dhidi ya wakulima.


Alisema kuwa, vitendo hivyo vimechangia kuwakatisha tamaa wakulima ambao wengi wao walishakataa kurudi tena kulima zao hilo, lakini  kutokana na hatua nzuri ya serikali kuanza kuwachukulia hatua wezi hao hivi sasa baadhi ya wakulima wamekubali kuanza tena uzalishaji wa zao hilo, ambalo miaka ya nyuma lilikuwa mkombozi mkubwa kiuchumi kwa wananchi wa Namtumbo.

Katika hatua nyingine Mkurugenzi huyo alieleza kuwa halmashauri imeanza mkakati wake wa kulima zao la kahawa na kwamba zaidi ya miche 16,000 imenunuliwa kutoka kituo cha utafiti wa kahawa cha Ugano, kilichopo wilayani Mbinga mkoani humo na kusambaza kwa wakulima katika kata ya Namabengo na Msindo.

Alifafanua kuwa lengo la  Halmashauri hiyo, ni kwamba kuwa na mazao matano ya biashara ambayo yatasaidia wananchi kuondokana na umaskini kwa sababu watakuwa na mazao mengi ya biashara, badala ya kutegemea zao la tumbaku na ufuta.

Mpenye aliyataja mazao hayo ni ufuta, mbaazi, korosho, kahawa na mhogo ambapo kwa mwaka ujao wanatarajia kuongeza mazao mengine mawili ambayo ni ya choroko na viazi vitamu hivyo tayari Halmashauri, imetenga zaidi ya shilingi milioni 200 kwa ajili ya kuendeleza shughuli za kilimo wilayani humo.

Pamoja na mambo mengine, wakulima wa wilaya ya Namtumbo wamehimizwa pia kulima zao la ufuta mweupe  ambalo litawaingizia kiasi kikubwa cha fedha kutokana na zao hilo, kuwa na soko kubwa  ndani na nje ya nchi.

Halmshauri hiyo imekwisha toa  mbegu 560 bure za ufuta na kuzigawa kwa wananchi, ili waweze kufanya uzalishaji wa zao hilo la ufuta.


Alizitaja kata zilizopata mgao huo kuwa ni Mchomoro, Namtumbo, Mgombasi, Luchiri, Mkongo, Limamu, Likuyu seka, Rwinga, Litola, Ligera na Namabengo ambapo  hivi sasa mashamba yanaendelea vizuri na kinachosubiriwa ni kazi ya ukataji  na ukaushaji kabla ya kufungua rasmi soko la zao hilo katika maeneo mbalimbali ya wilaya ya Namtumbo.

No comments: