Thursday, May 5, 2016

MADIWANI HALMASHAURI MJI WA MBINGA WALIA NA WALIMU KUKIMBILIA MJINI

Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, limemtaka Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Oscar Yapesa kuchukua hatua ya kuhamisha walimu wa shule za msingi na sekondari ambao wengi wao wapo katika shule za mjini huku zilizopo pembezoni mwa mji huo, zikiwa hazina walimu wa kutosha jambo ambalo linakwamisha maendeleo ya taaluma katika shule hizo.

Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Senyi Ngaga.
Madiwani hao walisema kuwa mwalimu mmoja hulazimika kufundisha vipindi vingi vya masomo darasani, huku wakitolea mfano shule ya msingi Changarawe iliyopo katika kata ya Mpepai ambayo ina walimu wawili tu, kutoka darasa la kwanza hadi la saba.

Hayo yalisemwa na Madiwani hao walipokuwa kwenye baraza la mji huo ambalo liliketi mjini hapa, ambapo pamoja na mambo mengine walisisitiza kuwa walimu waliopo mashuleni wanapaswa kujitolea kufundisha kwa moyo katika maeneo yao ya kazi, ili kuweza kuleta matokeo mazuri kwa watoto wanaosoma katika shule hizo.

“Mheshimiwa Mwenyekiti sijafurahishwa kabisa na mwenendo huu wa watumishi hawa wa idara elimu, kuwa na tabia ya kuhama na kukimbilia hapa mjini huku shule zetu zilizopo pembezoni wanafunzi wakiwa wanateseka kutokana na kukosa vipindi vya masomo darasani, hali hii inapaswa kudhibitiwa kuanzia sasa na walimu waliorundikana hapa mjini waondolewe na kwenda kuziba pengo la shule za pembezoni mwa mji wetu”, alisema Benedict Ngwenya Diwani wa kata ya Mpepai.


Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri hiyo, Yapesa alikiri kuwepo kwa madai hayo ya Madiwani na kueleza kuwa hatua za utekelezaji zitafanyika haraka ili kuweza kuondoa kero hiyo.

“Kwa kweli hali ni mbaya, tusipochukua hatua mapema hatutaweza kuleta matokeo mazuri katika maendeleo ya taaluma shuleni, jambo hili nitakuwa mkali sitazembea katika kulisimamia”, alisema Yapesa.


Kadhalika Yapesa aliwataka viongozi waliopo katika idara ya elimu Halmashauri ya mji wa Mbinga, kuanzia sasa kufanya uhakiki wa walimu waliopo katika shule za mjini na endapo kutakuwa na zidio la walimu apewe taarifa mapema ili waweze kwenda kuziba pengo la uhaba wa walimu, katika shule zilizopo pembezoni mwa mji huo.

No comments: