Friday, May 13, 2016

TAKUKURU YAWATAKA WAANDISHI WA HABARI KUFANYA KAZI ZAO KWA WELEDI



Na Kassian Nyandindi,
Songea.

WAANDISHI wa habari mkoani Ruvuma, wametakiwa kusaidia juhudi zinazofanywa na Rais Dkt. John Magufuli katika kuwafichua watumishi wa umma ambao wanajihusisha na vitendo vya rushwa na ufisadi, ambavyo vinachangia kurudisha nyuma kasi ya  kuleta maendeleo kwa wananchi.
Yustina Chagaka.

Aidha imeelezwa kuwa, vitendo hivyo vinavyofanywa na watumishi hao hasa katika miradi  ya maendeleo inakwamisha malengo ya serikali katika kupunguza tatizo la umaskini kwa baadhi ya maeneo hapa nchini, kwani miradi inayosimamiwa au kutekelezwa na wala rushwa inajengwa chini ya kiwango na hivyo kushindwa kuleta tija iliyokusudiwa.

Hayo yalisemwa hivi karibuni na Mkuu wa Taaisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Ruvuma, Yustina Chagaka wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini Songea.


Alisema kuwa vitendo vya rushwa, imekuwa ni kero kubwa katika jamii hivyo kila mmoja anapaswa kuhakikisha anatoa ushirikiano wa kutosha kwa taasisi hiyo, ili wahusika waweze kuchukuliwa hatua ikiwemo kuwafikisha Mahakamani.

“Tumieni kalamu zenu kuwafichua watumishi wa umma, wanaojihusisha na vitendo vya rushwa katika mkoa wetu, wao ndiyo kikwazo kikubwa cha kuongeza umaskini  hapa nchini, waandishi wa habari mnayo nafasi kubwa ya kuwabaini watu hawa”, alisema Chagaka.

Kwa mujibu wa Chagaka aliongeza kuwa waandishi wa habari wakitumia vizuri kalamu yao wana nguvu kubwa kuliko kitu chochote, kwani wanao uwezo wa kumfikia kila mtu katika jamii na popote pale wanapoishi.

No comments: