Tuesday, May 3, 2016

MAHAKAMA YADAIWA KUMWACHIA HURU MBAKAJI

Na Steven Augustino,
Tunduru.

MAHAKAMA ya wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, imemwachilia huru Mmanga Abdalah Hamdani (47) ambaye ni mtuhumiwa wa kosa la ubakaji, mtoto wa miaka 13 wa darasa la sita shule ya msingi Nanjoka wilayani humo.

Akitoa hukumu hiyo Hakimu mkazi mfawidhi Mahakama hiyo, Gladys Barthy alisema kuwa mahakama hiyo imechukua hatua hiyo baada ya kujiridhisha na ushahidi uliotolewa na wataalamu wa utabibu, mganga wa hospitali ya serikali ya wilaya ya Tunduru Dkt. Gaofrid Mvile kuwa mtoto huyo hakubakwa.

Akifafanua hukumu hiyo, Hakimu huyo alisema kuwa kufuatia hali hiyo mahakama imeamua kutenda haki kwa kutoa uamuzi huo wa kumwachilia huru kwa madai kwamba, huenda binti huyo alimsingizia mbakaji huyo ambaye ni mjomba wake kwa lengo la kutaka kumkomoa.

Akinukuu taarifa ya ushahidi uliotolewa na Dkt. Mvile, Hakimu huyo alisema kuwa taarifa zinaeleza kuwa hadi siku wanamfanyia vipimo vya ukaguzi wa kuthibitisha tukio hilo la ubakaji, malalamikaji hakuonesha kuwa na dalili za kuingiliwa na badala yake alionekana kuwa na bikra yake na kwamba kilichobainika katika uchunguzi huo ni uwepo wa mrundikano wa damu, ambazo zilitolewa kwa kumfanyia upasuaji wa tumbo lake.


Kwa mujibu wa taarifa za awali za tukio hilo, zinaeleza kuwa mtuhumiwa huyo alikuwa na tabia ya kumuingilia kimapenzi mtoto huyo ikiwemo pia kinyume cha maumbile, katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

Awali akimsomea shitaka hilo lenye jalada namba 23/2016, mbele ya hakimu wa mahakama hiyo, mwendesha mashtaka wa Polisi Inspekta Songelaeli Jwagu alisema kuwa mtuhumiwa huyo alitenda kosa hilo, February 21 mwaka huu majira ya saa  4.40 usiku baada ya kumvamia na kumziba mdomo mtoto huyo na kufanikisha adhma hiyo.

Alisema kwa kufanya hivyo, alifanya kosa kinyume cha sheria namba 130 (1) na (2c) ya kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyofanyiwa mabadiliko mwaka 2002.

Katika utetezi wake mtuhumiwa huyo katika kuthibitisha kuwa hakufanya kosa hilo, alipeleka mahakamani hapo mashahidi watatu huku Daktari huyo ambaye alipelekwa na upande wa Jamuhuri  kati ya mashahidi wake watano ili kuweza kuthibitisha hilo.

Wakizungumzia adhabu hiyo nje ya mahakama, mama mazazi wa mtoto huyo Fatuma khalifa Msaka na  bibi wa mtoto huyo Zaituni Rashid walidai kuwa hukumu hiyo haijawatendea haki, hivyo kutokana na wao ni familia maskini wanamwachia Mungu.

Walisema uwepo wa matumizi mabaya ya fedha (Rushwa) ulianza kujionesha tangu mwanzoni mwa kesi hiyo baada ya Polisi katika kituo cha wilaya hiyo, kumwachilia huru mtuhumiwa jambo ambalo liliwafanya kulalamika kwa  Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Ruvuma, Zubery Mwombeji ambaye aliingilia kati suala hilo na kutoa msukumo wa kumkamata tena mtuhumiwa huyo na kesi yao kwenda mahakamani.

Walisema shauri hilo lilifunguliwa February 21 mwaka huu na kupewa namba TUR/IR/202/2016 lakini kilichowashangaza mtuhumiwa huyo aliachiliwa kwa dhamana, wakati mgonjwa akiwa bado amelazwa hospitali na hali yake ikiwa mbaya.

Katika maelezo ya nyongeza, bibi Rashid alisema kuwa kutokana na mjukuu wake kufanyiwa tukio hilo na kuharibiwa vibaya katika maumbile yake ya uzazi, hivi sasa amekuwa akitokwa na kinyesi na haja ndogo bila kujizuia.

Wanafamilia hao wameiomba serikali, taasisi na mashirika ya kusimamia haki za wanawake na watoto kuwasaidia kwa kuwapatia usimamizi wa karibu ili kesi hiyo iliyovurugwa kwa nguvu ya fedha, ifufuliwe upya ili mtoto huyo aweze kupata haki zake za msingi.


Kwa mujibu wa taarifa za wanafamilia hao zinaeleza kuwa, mtuhumiwa Hamdani alianza kuishi na mtoto huyo mwaka 2013 baada ya shangazi wa mtoto huyo ambaye ni mke wa mtuhumiwa huyo, aliyetajwa kwa jina la Khadija  Pemba kwenda kumchukua katika kijiji cha Namasakata wilayani Tunduru kwa lengo la kuishi naye.

No comments: