Sunday, May 29, 2016

WAVUVI WAMTAKA RAIS MAGUFULI KUMCHUKULIA HATUA MKURUGENZI MTENDAJI WILAYA YA NYASA

Rais John Magufuli.


Na Muhidin Amri,
Nyasa.

MAISHA ya wavuvi katika  mji wa Mbambabay wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma yako hatarini, kufuatia wavuvi hao kutumia maji ya ziwa Nyasa ambayo sio safi na salama kwa ajili ya kunywa na matumizi mengine ya kawaida, katika maisha yao ya kila siku.

Imeelezwa kuwa hali hiyo inatokana na kukosekana kwa huduma hiyo ya maji katika eneo wanalofanyia shughuli zao za biashara ya kuuza samaki.

Wavuvi hao pia wameilalamikia Ofisi ya maliasili na uvuvi wilayani humo kwa kushindwa kupeleka huduma hiyo na miaka mingi sasa imepita, kwa ajili ya matumizi  ya wavuvi na wananchi wengine wanaofika kwa ajili ya kujipatia kitoweo cha samaki na kufanya shughuli  zao za kujiongezea kipato.

Kutokana na hali hiyo, kuna uwezekano mkubwa wa eneo hilo kukumbwa na magonjwa hatari ya mlipuko au kuambukiza kama vile kuhara, kipindupindu na magonjwa ya matumbo ambayo ni hatari kwa maisha ya binadamu.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wavuvi hao  walisema kuwa, Ofisi husika katika Halmashauri hiyo haina msaada wowote kwa wavuvi kwani hata pale inapotokea dharura ziwani  ya watu kuzama maji, wao wenyewe ndiyo wanaofanya jitihada ya kujiokoa wenyewe.


Walifafanua kwamba, kila wanapoomba boti  ili waweze kwenda kuwaokoa wenzao hulazimishwa kuweka mafuta kiasi cha lita 30 hadi 50 kwenye boti ya serikali kwa kutumia fedha zao za mfukoni, jambo ambalo limekuwa ni kero kubwa kwao.

Pia waliongeza kuwa ni haki yao kutumia chombo hicho cha serikali, lakini ugumu wanaoupata unatokana na watendaji husika kutowajali wavuvi hao ambao wanamchango mkubwa ndani ya wilaya ya Nyasa.

Kadhalika walisema bado wanakutana na  vikwazo vingi kutoka idara ya uvuvi na maliasili, lakini kinachowasikitisha hasa pale wanapoona boti hilo hutumika tu kuwasaka wavuvi haramu.

Waliongeza kuwa hata huduma ya choo iliyopo katika eneo hilo la mwambao wa ziwa Nyasa, imejengwa kwa michango ya wavuvi na wachuuzi hao ambao walichangishana fedha, baada ya kuona wanapata taabu ya kupata huduma  hiyo muhimu.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, mchuuzi wa dagaa Fatuma Mulemule ameiomba serikali kupitia Waziri mwenye dhamana sekta ya uvuvi na maliasili kuwachukulia hatua maafisa wao ambao ni kikwazo katika shughuli za maendeleo ya wananchi.

Mulemule alisema kuwa idara ya uvuvi imekuwa ikihusika na kukamata  mazao ya samaki kutoka kwa wavuvi kwa maelekezo ya Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri hiyo, Jabir Shekimweri bila kufuata taratibu ikiwemo pale wanapotoza ushuru wakati mwingine wamekuwa hawatoi stakabadhi halali ya serikali.

Kwa mujibu wa Mulemule ni kwamba taarifa hizo wamezikifisha kwa Mkurugenzi huyo, Shekimweri lakini cha kushangaza hakuna hatua aliyoichukua dhidi ya watumishi wake wanaohusika kufanya hivyo.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa umoja wa wavuvi wilayani Nyasa Morice Mkinda alisema ni jambo la aibu kuona halmashauri ya wilaya  inashindwa kupeleka huduma ya maji kwenye eneo hilo ambalo linatumiwa na wavuvi hao, huku wakiendelea kutoza ushuru kila kukicha.

Mkinda alieleza kuwa Mkurugenzi huyo hana ushirikiano na wavuvi ambapo kila wanapohitaji kukutana naye amekuwa akiwapiga chenga, jambo linaloonesha kwamba anafanya kazi kwa mazoea hivyo kuna kila sababu kwa Rais Dkt. John Magufuli kutengua uteuzi wake kwani tayari anaonekana kushindwa kusimamia kikamilifu maendeleo ya wilaya hiyo.

“Huyu Mkurugenzi ni vyema Mheshimiwa Rais akamuondoa katika wilaya yetu, huu ni mzigo kweli kweli, hana msaada wowote kwetu ndiyo maana  anashindwa hata kusimamia na kutekeleza majukumu aliyopewa na viongozi wake wa ngazi ya juu”, alisema Mkinda.

Akijibu tuhuma hizo Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo ambaye pia ni Mhandisi wa maji  wa wilaya hiyo, Evaristo Ngole alisema kuwa matatizo hayo yatafanyiwa kazi na kwamba kuhusiana na tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama katika eneo hilo la wavuvi, wanategemea kuanza kupeleka huduma hiyo katika eneo hilo baada ya mchakato wa kupata fedha kwa ajili ya utekelezaji.

“Suala hili la maji kimsingi tunatarajia kuanza kulifanyia kazi mwezi ujao mara baada ya kukamilika taratibu za kifedha, tayari Ofisi ya Mkurugenzi imeanzisha mchakato wa kuweza kupata fedha za kujenga miundombinu ya maji safi na salama, hatutaki wale wenzetu waendelee kutaabika”, alisema Ngole.

Naye afisa maliasili na uvuvi wa wilaya hiyo, Dkt. Stephen Madondora alikanusha madai ya wavuvi hao kwamba wanawatoza mafuta kwa ajili ya kwenda kufanya uokoaji pale kunapotokea matatizo ziwani huku akisisitiza kwamba,  wamekuwa wakitoa msaada mara kwa mara kwa wavuvi hao na watu wengine bila kuwadai chochote.

Madondora alisema serikali tayari  imeandaa boti sita ambazo zitatumika katika ziwa hio upande wa Nyasa, na kwamba pamoja na kufanya kazi ya doria pia itatumika kwa ajili ya kuokoa wananchi ambao watapata matatizo wakiwa ndani ya maji.

No comments: