Friday, May 20, 2016

DED MBINGA AWATAKA VIONGOZI KUWA WAADILIFU


Mkurugenzi mtendaji Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Venance Mwamengo upande wa kushoto, akizungumza na wakulima wa zao la Mhogo kijiji cha Kigonsera kata ya  Kigonsera wilaya humo ambapo aliahidi kuwasaidia fedha, kwa ajili ya kununulia mashine ya kisasa kusindika zao hilo na mazao mengine.
Na Mwandishi wetu,
Mbinga.

MKURUGENZI Mtendaji Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma Venance Mwamengo, amewataka viongozi waliopo katika vikundi  vya  wakulima wilayani humo kuwa waaminifu na waadilifu ili kuvifanya vikundi hivyo viweze kufikia malengo yake yaliyokusudiwa na kuweza kupunguza kero na matatizo mbalimbali, yanayowakabili wakulima waweze kuondokana na umaskini au ukosefu wa ajira.

Mwamengo alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki, alipokuwa akizungumza na wakulima wa kikundi cha Jitegemee ambacho hujishughulisha na kilimo cha mbaazi, mhogo, mahindi na alizeti katika kijiji cha Kigonsera wilayani humo huku akisisitiza kwamba  uaminifu wa viongozi hao utasaidia kwa kiasi kikubwa vikundi hivyo kuwa endelevu.

Alisema serikali imekuwa  ikivisaidia fedha na hata ushauri kwa kuwapeleka huko watalaamu wake, lakini tatizo kubwa lililopo viongozi wasiotambua wajibu wao katika vikundi wamekuwa kikwazo kikubwa kutokana na kutaka kujinufaisha kupitia mgongo wa wenzao kwa manufaa yao binafsi,  jambo ambalo huchangia kwa kiasi kikubwa visiweze kusonga mbele.


Kadhalika amewataka wakulima kutokatishwa tamaa kutokana na changamoto wanazokutana nazo katika sekta ya kilimo, bali waendelee kuongeza juhudi na uzalishaji wa mazao shambani ili waweze kupiga hatua mbele kiuchumi.

Aidha Mwamengo, amesikitishwa na tabia ya baadhi ya watu kutumia muda wao mwingi kukaa vijiweni  kucheza bao au kunywa pombe saa za kazi  badala ya kujikita zaidi katika shuguli za maendeleo, ambapo alisema serikali  itahakikisha  inawakamata na kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria ili kuonesha kwamba kuna umuhimu  wa mtu kufanya kazi.

Alisema kuwa kila kaya ni lazima iwe na mipango thabiti ya kukabiliana na umaskini, hatua ambayo itasaidia kuinua hali zao za maisha  na sio kugeuka  kuwa  watazamaji au mabingwa wa kulalamika na kuelekeza lawama zao kwa serikali.

Katika hatua nyingine, halmashauri ya wilaya ya Mbinga kupitia idara ya kilimo  katika msimu wa kilimo wa mwaka 2015/2016  imefanikiwa kugawa mbegu za mbaazi kilo 8,000 kwa wakulima wa wilaya hiyo, ambazo tayari zimeshapandwa katika msimu wa kilimo wa mwaka huu.

Pamoja na mambo mengine, Ofisa mazao  wa wilaya hiyo Deodatus Kisima alieleza kwamba lengo la mpango huo ni kuwasaidia wakulima  waweze kufanikisha malengo yao katika shughuli zao za kilimo, hatua ambayo itawafanya wajiinue kiuchumi kutokana na  kulima kwa njia ya kisasa na kutumia mbegu bora zinazozaa vizuri, ili kuepusha hatari ya kutumia mbegu zisozofaa.

No comments: