Sunday, May 15, 2016

WAKULIMA MBINGA WAIOMBA SERIKALI KUWAPATIA MASHINE YA KUSINDIKA ZAO LA MHOGO

Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

WAKULIMA wa zao la Mhogo katika kijiji cha Kigonsera kata ya Kigonsera wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wameiomba serikali kuangalia uwezekano wa kuwapatia mashine ya kusindika  zao hilo na mazao mengine wanayolima, ili waweze kuongeza thamani ya uzalishaji na kuwafanya waweze kupata soko la uhakika la kuuzia mazao yao.

Hayo yalibainishwa hivi karibuni na wakulima hao, walipokuwa wakizungumza na mwandishi wetu  wakiwa kwenye shamba darasa  la mhogo  linalotumika kwa ajili ya kufundishia wakulima kutoka maeneo mbalimbali ya wilaya ya Mbinga na wakulima wa wilaya nyingine za mkoa huo, juu ya kilimo bora cha mhogo.

Katibu wa kikundi cha Jitegemee, Oscar Ndunguru alisema kuwa wamekuwa wakulima wazuri  wa zao la mhogo na mazao mengine ya chakula na biashara  kutokana na elimu wanayoipata kutoka kwa maofisa ugani, ambapo changamoto kubwa wanayokabiliana nayo sasa ni ya ukosefu wa mashine hiyo ya kusindika mazao wanayozalisha, jambo ambalo linasababisha wakose soko la uhakika la kuuzia mazao yao.

“Tumekuwa wakulima wazuri ambao tunafuata kanuni bora za kilimo hiki cha mhogo, bado tatizo kubwa linalotukabili hapa kwetu ni ukosefu wa soko la uhakika ambalo linachangiwa kwa kiasi kikubwa kutokana na ukosefu wa mashine ya kisasa ya kusindika zao hili, ili tuweze kuongeza thamani”, alisema Ndunguru.


Alisema kuwa, wakati umefika kwa serikali kupitia halmashauri ya wilaya ya Mbinga, kuona umuhimu wa kuwasaidia wakulima hao kwa kuagiza mashine nyingi za kusindika mazao mbalimbali yanayozalishwa wilayani humo, ili kuweza kuwafanya wakulima waweze kuondokana na umaskini.

Naye mkulima aliyejitambulishwa kwa jina la Nuhu Kisoma, alieleza kuwa wamekuwa pia wakizalisha mazao mengine ya chakula na biashara kama vile alizeti, mhogo, mahindi na mbaazi.

Alisema kuwa endapo serikali itawathamini  wakulima na kuwaunga mkono  katika shughuli zao kwa kuwanunulia mashine za usindikaji mazao wilayani humo, wataweza kupiga hatua mbele badala ya kusubiri wateja wachache ambao huwafuata mashambani mwao na kuwarubuni kuwauzia mazao yao, kwa bei ndogo ambayo hailingani na gharama ya uzalishaji.

Kwa upande wake Meneja wa shirika la SIDO mkoa wa Ruvuma, Emmanuel Makele aliwataka wakulima hao kuongeza jitihada katika uzalishaji wa mazao hayo na kujiunga katika vikundi vya ujasiriamali, ili serikali iweze kuwafikia kwa urahisi katika utoaji wa huduma zake.


Makele alisema, kuna kila sababu kwa wananchi kutumia fursa  ya ardhi waliyonayo hapa nchini kwa kujikita zaidi katika shughuli za kilimo badala ya kusubiri msaada kutoka serikalini, kwani tabia hiyo  inaweza kuchelewesha  maendeleo yao na kutofikia malengo  yaliyokusudiwa.

No comments: