Friday, May 20, 2016

WAKULIMA WA KAHAWA WASHAURIWA KUTUMIA MICHE YA VIKONYO



Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

WAKULIMA wanaozalisha zao la kahawa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, wameshauriwa kuendelea kutumia miche bora ya kahawa aina ya vikonyo ambayo haishambuliwi na wadudu waharibifu kwa urahisi na wakati wa mavuno, huwafanya waweze kupata mazao mengi shambani.

Aidha Taasisi ya utafiti wa zao la kahawa (TaCRI) wilayani humo, imepongezwa kwa jitihda zake inazoendelea kuzifanya, kwa kutoa elimu kwa wakulima wa zao hilo hususan katika uzalishaji wa miche hiyo bora ya kahawa ambayo huwaletea tija kubwa wakulima na kuwafanya waondokane na umaskini.

Hayo yalisemwa na mkulima mmoja maarufu wa zao hilo kutoka kijiji cha Sepukila kata ya Kilimani wilayani hapa, Festo Mapunda alipokuwa akihojiwa na waandishi wa habari juu ya uendelezaji wa kilimo bora cha zao hilo katika wilaya ya Mbinga.

“Mimi binafsi naishukuru taasisi hii ya TaCRI, kwa kutupatia elimu ya kilimo bora cha kahawa, hivi sasa wakulima tunaweza kuzalisha miche ya vikonyo na kutoa ushauri juu ya kilimo bora cha zao hili kwa wengine ambao wanapenda kulima kahawa”, alisema Mapunda.


Mapunda aliongeza kuwa yeye ana ekari nne za kahawa bora, ambazo huzalisha zao hilo kwa wingi kila mwaka na kwamba kwa upande wa uzalishaji wa miche ya vikonyo, ameanzisha shamba darasa ambalo linawanachama 42 wanaojishughulisha na uzalishaji wa zao hilo.

Alisema kuwa shamba darasa hilo linafahamika kwa jina la Mitenga, limesajiliwa kisheria ambapo uzalishaji wa miche hiyo wamekuwa wakiufanya kila mwaka kwa ajili ya kuwauzia wakulima wengine.

Pia alifafanua kuwa pamoja na kujikita katika uzalishaji wa zao hilo, vilevile wamekuwa wakijishughulisha na kazi ya utunzaji wa mazingira kwa kupanda miti rafiki ya maji, kwenye vyanzo vya maji na vilele vya milima.

Hata hivyo alibainisha kwamba hivi sasa wana shamba la miti zaidi ya ekari 10 hivyo ametoa mwito kwa wananchi wengine kujitokeza kwa wingi na kwenda kujifunza shughuli za kilimo bora cha kahawa na upandaji wa miti, unaofanywa na kikundi hicho cha shamba darasa Mitenga kilichopo katika kijiji cha Sepukila kata ya Kilimani wilayani Mbinga.

No comments: