Sunday, May 29, 2016

WARATIBU ELIMU KATA WATAKIWA KUKUSANYA TAKWIMU SAHIHI

MKuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu.


Na Joyce Joliga,
Songea.

WARATIBU elimu kata katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, wameshauriwa kuhakikisha kwamba wanasimamia kikamilifu zoezi la ukusanyaji  takwimu kwa umakini mkubwa ili kuweza kupata usahihi wa takwimu za idadi ya wanafunzi kwa kila shule za msingi, ziweze kusaidia kuhakikisha vyandarua vinavyogawiwa kwa wanafunzi hao vinatumika kwa walengwa husika, kwani ikibainika kutoa takwimu za uongo watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Agizo hilo limetolewa juzi na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa hiyo, Jenifer Christian wakati alipokuwa akifungua mafunzo ya siku moja ya  mpango wa ugawaji vyandarua mashuleni, yaliyofanyika mjini hapa.

Hii ni awamu ya nne kwa Waratibu kata, zaidi ya 30 toka Halmashauri tatu za Manispaa ya Songea, Madaba, pamoja na wilaya ya Songea kupata vyandarua hivyo ambapo mafunzo hayo yaliandaliwa na shirika lisilo la kiserikali la PSI.


Alisema kuwa mafunzo hayo yawe msasa na kuwafanya wafanye kazi kwa weledi mkubwa ili kulifanya zoezi hilo kuwa na mafanikio, ufanisi mkubwa kwani mpango huo una lengo la kulinda umiliki wa vyandarua katika ngazi ya kaya ambao umefanikiwa kwa asilimia 85.

Jenifer alisema kuwa katika awamu ya tatu, watoto kuanzia darasa la kwanza hadi la saba waliweza kupewa vyandarua ambapo jumla ya vyandarua 494,407 walivigawa katika mikoa mitatu ambapo kwa mkoa wa Ruvuma, mahitaji yalikuwa vyandarua 188,851.

Mpango huo wa ugawaji wa vyandarua kwa jamii, kupitia watoto hao waliokuwa  katika shule za msingi ni utaratibu uliobuniwa na serikali kwa kushirikiana na Wizara tatu za Ofisi ya Rais TAMISEMI, Wizara ya afya maendeleo ya jamii jinsia, wazee na watoto pamoja na Wizara ya elimu kwa lengo la kuhakikisha jamii inapata vyandarua vya kutosha na waweze kujikinga na ugonjwa hatari wa malaria.

Kwa upande wake  Mratibu wa mradi wa PSI mkoa wa Ruvuma na Njombe Wilfredy Mkungilwa alisema kuwa endapo wanafunzi hao watapatiwa vyandarua hivyo, kwa kiasi kikubwa itasaidia kupunguza vifo vinavyotokana na ugonjwa huo.

No comments: