Sunday, May 29, 2016

WAKULIMA TUNDURU WATAKIWA KUFUATA MAELEKEZO YA WATALAAMU WA UGANI



Na Steven Augustino,
Tunduru.

WAKULIMA wanaozalisha mazao ya aina mbalimbali wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, wametakiwa kufuata maelekezo wanayopewa na wataalamu wa ugani wa wilaya hiyo ili waweze kujiletea maendeleo katika sekta ya kilimo na kuondokana na umaskini uliokithiri miongoni mwao, ambao umekuwa ukiwasumbua kwa miaka mingi katika maeneo ya vijiji vyao wanavyoishi.

Mwito huo ulitolewa na mwakilishi wa Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Tunduru, Afisa kilimo wa Halmashauri hiyo Chiza Marando wakati akizungumza na vikundi vya wakulima kutoka vijiji vya Legezamwendo, Kidodoma, Machemba na Mkwajuni.

Aidha Marando alisema kuwa mtindo wakati wote kuwalaumu wataalamu hao ambao umekuwa ukifanywa na wananchi wengi katika vijiji wilayani humo, hauwezi kuwasaidia na kwamba kinachotakiwa waitikie wito na kusikiliza maelekezo wanayopewa ili waweze kuzalisha mazao bora.


Alisema katika kuhakikisha kwamba serikali imejipanga kuwapelekea maendeleo, Halmashauri yake kupitia miradi mbalimbali inayotekelezwa tayari imeanza kuwajengea miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji katika maeneo yao, pamoja na kuwawekea mashine ya kukoboa mpunga kwa madaraja kwa lengo la kuongeza thamani ya mazao yao.

Marando aliyataja maeneo waliyojenga miundombinu hiyo kuwa ni katika maeneo ya Madaba, Legezamwendo, Lelolelo, Kitanda na Misyaje wilayani Tunduru.

Kuhusu mashine ya kukoboa mpunga kwa madaraja alisema kuwa imefungwa katika eneo la Nakayaya Tunduru mjini, eneo ambalo kila mkulima anaweza kufika kwa urahisi na kupata huduma husika.

Alisema hata hivyo uzoefu unaonesha kwamba soko lipo kubwa la zao la mpunga ambao hukobolewa kwa wingi na kuwekwa kwenye daraja la kwanza  ambao hufungwa katika vifungashio maalumu, ambavyo vimethibitishwa na shirika la Viwango Tanzania (TBS) ambapo huuzwa shilingi 3,000 kwa kila kilo moja kwa mchele wa daraja hilo la kwanza.

Kwa mujibu wa Marando aliongeza kuwa mikakati mingine waliyojiwekea ni pamoja na Halmashauri yake kuweka utaratibu wa wakulima hao kuuzia mazao yao katika maeneo yaliyoainishwa, lengo ikiwa ni kuisaidia serikali kukusanya takwimu ambazo zitaweza kusaidia kupanga mikakati thabiti ya kuwahudumia wakulima wake kwa kutumia takwimu sahihi.

No comments: