Sunday, May 29, 2016

NYASA WALALAMIKIA KUNYANYASWA WANAPOHITAJI HUDUMA ZA MATIBABU



Na Muhidin Amri,
Nyasa.

BAADHI ya wajasirimali wadogo wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma, wamesema wanashindwa kujiunga  na mfuko wa Taifa wa bima ya afya (NHIF) na mfuko wa afya ya jamii (CHF) kutokana na  manyanyaso wanayopata wanachama wa mfuko huo, pale wanapokwenda katika  zahanati na vituo vya kutolea huduma za matibabu wilayani humo.

Walisema kuwa wanapenda kujiunga na mpango huo wa huduma za afya, NHIF na CHF lakini tatizo kubwa linalowafanya wasite kujiunga na mifuko hiyo ni pale wanaposhuhudia wenzao ambao tayari wamejiunga, kutopata matibabu ya haraka kutokana na watoa huduma kwenye vituo hivyo kuwanyanyapaa kwa madai kwamba wanakosa fedha kutoka kwa watu ambao wanakuja na fedha taslimu kulipia matibabu.

Walitoa kauli hiyo hivi karibuni, wakati wa zoezi la uhamasishaji wajasiriamali wadogo ambao ni wateja wa Benki ya Wananchi Mbinga (MCB) wilayani humo ili waweze kujiunga na mpango huo, ambapo jumla ya wajasirimali 112 waliweza kujitokeza na kujiunga.


Akizungumza kwa niaba ya wenzake mmoja wa wajasiriamali hao, Joackim Kamanga alisema watumishi wa afya katika maeneo mengi ya kutolea huduma za matibabu wilayani Nyasa, wamekuwa na tabia ya kuwanyanyasa na kuwanyanyapaa wanachama wa mfuko wa afya ya jamii, hatua ambayo inachangia wananchi wengine kukataa kujiunga na mpango huo.

Kamanga alisema kuwa baadhi ya watumishi hasa wauguzi wana tabia mbaya ya kuchagua watu wa kuwahudumia kutokana na cheo au nafasi yake katika jamii, hivyo kukwamisha mpango huo wa serikali wa kuhamasisha wajasirimali wadogo walioko katika vikundi kuchangamkia fursa ya kujiunga na mpango huo wa  matibabu.

Katika hatua nyingine ameiomba Wizara ya afya, kuhakikisha kunakuwa na dawa za kutosha kwenye zahanati, vituo vya afya na hospitali zake ili wananchi waliokubali kujiunga na mfuko wa Taifa wa bima ya afya na ule wa afya ya jamii waweze kupata huduma bora za matibabu.

Naye Ofisa mikopo wa benki ya wananchi  Mbinga, ambao ndiyo wadhamini wa vikundi hivyo, Pirmin Nchimbi aliwataka wajasiriamali hao kutokuwa na hofu kuhusu mpango huo badala yake wachangamkie fursa hiyo iliyotolewa na serikali yenye lengo la kutoa huduma bora za matibabu kwa kila mtanzania.

Nchimbi aliongeza kuwa benki  ya MCB ipo tayari kuhudumia wateja wake na kwamba ina fedha za kutosha kwa ajili ya kuwakopesha  wajasiriamali wa aina mbalimbali, ili waweze kujiunga na kusonga mbele kimaendeleo.

Alisema kuwa katika utekelezaji wa mpango huo, benki hiyo ndiyo itahusika moja kwa moja kuingia mkataba na kulipa michango ya wajasiriamali wote ambao ni wateja wake,  ili nao waweze kuwa sehemu ya mafanikio ya mpango wa huduma bora za matibabu chini ya mfuko wa Taifa wa bima ya afya.

No comments: