Monday, May 30, 2016

TFDA YATEKETEZA BIDHAA FEKI NJOMBE



Na Kassian Nyandindi,
Njombe.

MAMLAKA ya Chakula, Dawa na Vipodozi (TFDA) Kanda ya nyanda za juu Kusini imeteketeza kilo 1,000 za bidhaa aina mbalimbali, Halmashauri ya wilaya na mji wa Njombe mkoani hapa, ambazo zimekwisha muda wa matumizi yake kwa binadamu zenye thamani zaidi ya shilingi milioni 10.

Uteketezaji wa bidhaa hizo unafuatia msako mkali ulioendeshwa na mamlaka hiyo kwa muda wa siku mbili, baada ya kupata taarifa kutoka kwa wasamaria wema kwamba maduka mengi yaliyopo mkoani humo baadhi yake yamekuwa yakiuza bidhaa zilizopitwa muda wa matumizi yake.

Kaimu Mkuu wa mkoa wa Njombe, Anatory Choya amewatahadharisha wananchi wa mkoa huo kuwa makini na bidhaa hizo huku akikemea tabia ya wafanyabiashara kuacha mara moja, kuuza bidhaa zilizopitwa na wakati kwani wamekuwa wakihatarisha usalama wa afya za watumiaji.

Aidha Choya alisema kuwa msako huo utakuwa endelevu kwa kupita kukagua kila duka lililopo mkoani humo, ikiwa pia ni lengo la kutokomeza kabisa tabia kwa baadhi ya wafanyabiashara wanaoingiza bidhaa hizo zilizopigwa marufuku na serikali.


Kaimu Mkuu huyo wa mkoa alisisitiza kwa kuwataka wataalamu wa TFDA kuendelea na zoezi hilo na kwamba, pale wanapowakamata wafanyabiashara wanaofanya hivyo wawafutie leseni zao za biashara ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo ya kuendelea kuuza bidhaa hizo.

''Niwatahadharishe wananchi na wafanyabiashara wote wa mkoa wa Njombe kitendo cha kuendelea kuuza bidhaa hizi feki ambazo zimepitwa na wakati ni kuwaumiza watumiaji, wafanyabiashara mnatakiwa kuacha tabia ya kuuza bidhaa zilizokwisha muda wake”, alisema Choya.

Choya alifafanua kwamba wafanyabiashara wengi wanaouza bidhaa hizo wamekuwa wajanja, ambapo wao wenyewe wamekuwa hawazitumii badala yake wamekuwa wakiwauzia wananchi kwa lengo tu la kutaka kupata faida jambo ambalo ni hatari kwa watumiaji.

Pamoja na mambo mengine, aliongeza kuwa kuna kila sababu kwa Mamlaka ya chakula, dawa na vipodozi hapa nchini kufungua ofisi zao katika kila mkoa na kujiwekea utaratibu wa kupitia mara kwa mara maduka ya wafanyabiashara, ili kuweza kudhibiti hali hiyo isiweze kuendelea kushamiri na kuumiza wananchi.

"Pale mnapobaini wafanyabiashara wanakiuka kanuni na sheria toeni taarifa kwenye vyombo vya dola, ili serikali iweze kuchukua hatua za kisheria kwa lengo la kuweza kudhibiti tabia hii ya wafanyabiashara kuendelea kuuza bidhaa zilizopitwa na wakati”, alisisitiza.

Naye Meneja wa Mamlaka hiyo Kanda ya nyanda za juu kusini, Rodney Alananga  alisema kuwa wamefanikiwa kukamata watu 57  katika Halmashauri ya mji na wilaya ya Njombe katika maduka yao, wakiuza bidhaa feki zilizopitwa na wakati.

Alisema kuwa katika msako huo walifanikiwa kukamata na kuteketeza majani ya chai, pipi za aina mbalimbali, maziwa ya watoto, vipodozi, vinywaji aina ya red bull na pombe kali aina ya viroba ambavyo vimetoka nchi jirani ya Malawi.

Hata hivyo Alananga alisema kuwa bidhaa zilizopita muda wake ni hatari kwa matumizi ya binadamu kwani zina sumu ambayo ni hatari kwa mtumiaji, huku akisisitiza kwa kuwataka wananchi wanapokwenda kununua bidhaa yoyote dukani kujenga mazoea ya kusoma mwisho wa tarehe ya matumizi, ili waweze kuepukana na madhara yanayoweza kuwapata hapo baadaye.

No comments: