Monday, July 20, 2015

MWANDISHI WA HABARI KASSIAN NYANDINDI ATANGAZA RASMI NIA YA KUGOMBEA UDIWANI KATA YA MBINGA MJINI A

Mwandishi wa habari Kassian Nyandindi, ambaye ametangaza nia ya kugombea udiwani katika kata ya Mbinga mjini A, iliyopo wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi. (CCM)
Na Dustan Ndunguru,
Mbinga.

KASSIAN Nyandindi ambaye amebobea katika fani ya uandishi wa habari, na sasa anaandikia gazeti la Majira mkoani Ruvuma, ametangaza nia yake ya kugombea udiwani katika kata ya Mbinga mjini A, iliyopo wilayani Mbinga mkoani humo kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Akizungumza leo na vyombo mbalimbali vya habari mjini hapa, Nyandindi alisema amekwisha chukua fomu ya kuwania nafasi hiyo na kuirejesha, huku akitamka vipaumbele vyake endapo wananchi wa kata hiyo watampatia ridhaa ya kuwaongoza, atahakikisha huduma muhimu za kijamii zinaboreshwa.

Alisema atazingatia kwamba miundombinu mbalimbali kama vile barabara za mitaa, afya, maji na elimu vinaboreshwa huku akisisitiza kuboresha elimu kutoka ngazi ya elimu ya msingi hadi sekondari kwa kuwataka pia wazazi kupeleka watoto wao shule na kuwapatia mahitaji muhimu ili mtoto aweze kusoma vizuri.  

“Uwezo wa kuongoza na kushughulikia matatizo ya wananchi wa kata hii ninao, kinachotakiwa hapa ni kutumia rasilimali tulizonazo ili tuweze kujipatia maendeleo na kuweza kuondokana na umasikini”, alisema Nyandindi.

Sunday, July 19, 2015

KALUMANGA MBIONI NA UBUNGE VITI MAALUM RUVUMA

Mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, Sondy Kalumanga kulia, akipokea fomu ya kuomba kugombea ubunge viti maalum kupitia tiketi ya CCM mkoani humo.

TINGA TINGA NA MIKAKATI YA MAENDELEO KATA YA MTIPWILI NYASA

Stanford Nyambo (Tinga tinga)
Na Dustan Ndunguru,

MWAKA huu unatarajiwa kufanyika uchaguzi mkuu ambapo Madiwani, Wabunge na Rais watachaguliwa na kuongoza kwa kipindi cha miaka mitano ijayo, ambapo uchaguzi huo utafanyika kwa kuvihusisha vyama ambavyo vimesajiliwa kisheria.

Chama Cha Mapinduzi (CCM) ndicho chama kinachoongoza nchi ya Tanzania kwa kipindi kirefu sasas, kwa kuhakikisha amani na utulivu kwa wananchi wake vinaendelea kuwepo.

CCM ni chama ambacho Watanzania wengi wanakiamini na kukichagua kushika dola tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992.

Watanzania hawa wameamua kwa dhati kuwachagua wagombea waliotokana na chama hiki tawala, kutokana na kuridhishwa na sera zake nzuri ambazo kimsingi zimekuwa zikilenga kuwaletea maendeleo wananchi, ikilinganishwa na sera za vyama pinzani.

KALOLO NA HARAKATI ZA KUPATA UBUNGE TUNDURU KASKAZINI

Ajili Kalolo, mgombea nafasi ya ubunge jimbo la Tunduru Kaskazini mkoani Ruvuma, akionesha fomu ya kugombea mara baada ya kuichukua kutoka ofisi za CCM wilayani Tunduru.
Na Steven Augustino,
Tunduru.
WANACHAMA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika jimbo la Tunduru kaskazini wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, wametakiwa kuwa makini na kutokubali kutumiwa na wajanja wachache wanaopita kuwanadi wagombea wanaowania nafasi ya ubunge katika majimbo ya uchaguzi wilayani humo, ambao wakishapata nafasi hiyo huondoka na kwenda kuishi mbali na majimbo yao.
Aidha wanachama hao ambao ni wakereketwa wa CCM, pia wametahadharishwa dhidi ya wagombea wa nafasi hiyo ambao wamekuwa na tamaa ya madaraka, hivyo wameshauriwa kuwachuja kwa hoja zao majukwaani, ili kuona kama kweli watakuwa na uwezo na moyo wa kuwasaidia wananchi pale watakapokuwa wamepewa nafasi ya kuwaongoza.
Hayo yalisemwa na kada wa Chama Cha Mapinduzi na afisa wa idara ya utawala na uwezeshaji  jumuiya ya wazazi  makao makuu ya chama hicho, Omary Kalolo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, mara baada ya chukua fomu ya kuwania nafasi ya ubunge katika jimbo hilo ambalo awali lilikuwa linaongozwa na mhandisi Ramo Makani.
Alisema kwamba licha ya kila mwanachama wa chama hicho, anayohaki ya kuchukua fomu na kuomba ridhaa ya kuingia katika kinyang’anyiro hicho, lakini wanapaswa kumchagua mtu makini na mwenye uwezo wa kuwaletea maendeleo wananchi wake na sio vinginevyo.

NDILIMALITEMBO SONGEA KUONGOZWA NA DIWANI MWANDISHI WA HABARI

Mgombea nafasi ya udiwani, kata ya Ndilimalitembo katika Manispaa Songea mkoani Ruvuma kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Cresencia Kapinga kushoto, ambaye pia ni mwandishi wa habari gazeti la Majira akijibu maswali kutoka kwa waandishi wa habari mara baada ya kuchukua fomu ya kuomba ridhaa ya kugombea nafasi hiyo katika kata hiyo.
Cresensia Kapinga akisindikizwa, ndugu na jamaa mara baada ya kutoka kuchukua fomu hiyo ya kuwania nafasi ya udiwani katika kata hiyo.


Saturday, July 11, 2015

AJINYONGA KUTOKANA NA KUDAIWA DENI

Na Mwandishi wetu,
Songea.

WATU wawili wamefariki dunia katika matukio tofauti, yaliyotokea wilayani Nyasa na Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, likiwemo la fundiseremala mmoja kujinyonga kutokana na kukimbia deni alilokuwa akidaiwa.

Akifafanua juu ya matukio hayo, Kamanda wa Polisi mkoani humo Mihayo Msikhela alisema tukio la kujinyonga lilitokea mtaa wa Ostarbey, katika kata ya Msamala Songea mjini.

Katika tukio hilo marehemu aliyefahamika kwa jina la PeterLufunda (38) alichukua hatua ya kujinyonga, baada ya Mahakama ya wilaya ya Songea kutoa hukumu ya kuiruhusu SACCOS ya mtaa huo kuuza nyumba yake aliyokuwa akiishi, ili kulipa deni la mkopo wa shilingi milioni 1 ambalo alikopa na kushindwa kulipa.

WAANDISHI NYANDA ZA JUU KUSINI WANOLEWA

Na Steven Augustino,
Lindi.

WAANDISHI wa habari Nyanda za juu kusini, wameshauriwa kufanya utafiti na kuandika habari zitakazofichua vitendo viovu vinavyofanywa na baadhi ya vigogo hapa nchini, ambao wamekuwa wakifanya biashara ya uvunaji misitu na kusafirisha kwa njia za panya jambo ambalo limekuwa likiikosesha serikali mapato yake.

Meneja kampeni ya mama misitu, Gwamaka Mwakyanjala alisema hayo alipokuwa akitoa mafunzo ya siku tano kwa waandishi wa habari wa mikoa ya Ruvuma, Mtwara na Lindi yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Lindi mkoani hapa.

Mwakyanjala alifafanua kuwa lengo la mafunzo hayo, ni kuwajengea uwezo waandishi wa mikoa hiyo waweze kuandika habari za misitu ili kusaidia kuibua mijadala ambayo itaiwezesha serikali, kutatua kero ambazo zimekuwa zikijitokeza juu ya uvunaji haramu wa misitu.

Tuesday, July 7, 2015

NYASA WAMPATA MRITHI WA KAPTENI KOMBA MJUMBE WA NEC


Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma, wakishangilia kwa pamoja kumpata mjumbe wa NEC wa wilaya hiyo Alex Shauri, mara baada ya uchaguzi kufanyika jana wilayani humo. (Picha na Kassian Nyandindi)
Na Kassian Nyandindi,
Nyasa.

WANACHAMA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Nyasa mkoa wa Ruvuma, wametakiwa kuwa makini kwa kutokubali kutumiwa na wagombea wanaowania nafasi ya ubunge wilayani humo hasa kwa wale ambao wamekuwa na tamaa ya madaraka, badala yake jukumu lao kubwa ni kuwachuja ili kuona kama kweli watakuwa na uwezo na moyo wa kuwasaidia wananchi, pale watakapokuwa wamepewa nafasi ya kuwaongoza.

Aidha wametakiwa kuhakikisha kwamba, CCM kinapata ushindi wa kishindo katika uchaguzi mkuu ujao unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25 mwaka huu, ambapo hilo litatokana na kujenga mshikamano wa dhati ikiwemo kutangaza kwa wananchi yale yote yaliyotekelezwa kwa vitendo na chama hicho, kama ilivyoainishwa ndani ya ilani yake ya uchaguzi.

Hayo yalisemwa na Mjumbe wa NEC wa wilaya ya Nyasa, Alex Shauri alipokuwa akiwashukuru wajumbe wenzake wa Chama Cha Mapinduzi wilayani humo, mara baada ya kumchagua kupeperusha bendera ya nafasi hiyo katika wilaya hiyo.

POLISI WAMSAKA BINTI ALIYETUPA KICHANGA CHOONI

Na Steven Augustino,
Songea.   

JESHI la Polisi wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wanamtafuta binti mwenye umri wa miaka 19 kwa lengo la kutaka kumfikisha kwenye vyombo vya sheria, ili aweze kujibu tuhuma za mauaji ya kichanga na mwili wake kuutumbukiza chooni.

Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Mihayo Msikhela alisema kuwa mtuhumiwa huyo alifanya unyama huo juzi na kutokomea kusikojulikana.

Msikhela alimtaja mtuhumiwa aliyefanya kitendo hicho kuwa ni, Germana Ndimbo mkazi wa kijiji cha Mkumbi kata ya Mkumbi wilayani humo ambapo alikuwa mjamzito na mara alipofanikiwa kujifungua, alichukua jukumu la kufanya unyama huo.

Sunday, July 5, 2015

WAJAWAZITO WAJIFUNGULIA MWANGA WA TOCHI YA SIMU

Kamanda wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma, akihutubia wananchi wa kata ya Linga wilayani humo hivi karibuni.
Na Kassian Nyandindi,
Nyasa.

AKINA mama wajawazito wanaopatiwa matibabu katika kituo cha afya Litumba kuhamba kata ya Linga, wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma wanapata shida wakati wa kujifungua nyakati za usiku, kutokana na kukosa nishati ya mwanga.

Kufuatia hali hiyo wauguzi wa kituo hicho cha afya, wanalazimika kutumia tochi za mwanga wa simu pale mama mjamzito, anapofikia hatua ya kutaka kujifungua.

Hayo yalisemwa na Muuguzi wa kituo hicho, Witness Mtende mbele ya Kamanda wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wilayani humo, Cassian Njowoka alipokuwa ametembelea kituo hicho kwa ajili ya kukabidhi msaada wa vifaa vya mfumo wa nishati ya umeme wa jua (Solar).

Mtende alisema pia wanakabiliwa na tatizo la ukosefu wa maji, nyumba za kuishi wahudumu wa afya hivyo wanaiomba serikali, ifanye jitihada ya kumaliza kero hiyo.

BIBIYE AGONGWA NA LORI AFARIKI DUNIA

Na Steven Augustino,
Tunduru.

MFANYABIASHARA mmoja ambaye ni maarufu kwa kuuza viazi vitamu, katika kitongoji cha Ng’apa kijiji cha Namiungo wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, Bibiye Yasin Mkao (43) amefariki dunia baada ya kugongwa na lori.

Chanzo cha ajali hiyo kimeelezwa kuwa kimetokana na dereva aliyekuwa akiendesha gari lenye namba za usajili, T 442 CBM ambalo ni mali ya kampuni ya kichina Synohdro, inayojenga barabara kwa kiwango cha lami kutoka wilaya ya Tunduru kwenda Mangaka mkoani Mtwara.

Diwani wa kata hiyo, Nurdin Mnolela alisema marehemu huyo aligongwa na lori hilo la kichina aina ya Howo Syno truck ambalo lilikuwa likiendeshwa na dereva, Noel Beda ambaye mpaka sasa ametokomea kusikojulikana.