Saturday, July 11, 2015

WAANDISHI NYANDA ZA JUU KUSINI WANOLEWA

Na Steven Augustino,
Lindi.

WAANDISHI wa habari Nyanda za juu kusini, wameshauriwa kufanya utafiti na kuandika habari zitakazofichua vitendo viovu vinavyofanywa na baadhi ya vigogo hapa nchini, ambao wamekuwa wakifanya biashara ya uvunaji misitu na kusafirisha kwa njia za panya jambo ambalo limekuwa likiikosesha serikali mapato yake.

Meneja kampeni ya mama misitu, Gwamaka Mwakyanjala alisema hayo alipokuwa akitoa mafunzo ya siku tano kwa waandishi wa habari wa mikoa ya Ruvuma, Mtwara na Lindi yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Lindi mkoani hapa.

Mwakyanjala alifafanua kuwa lengo la mafunzo hayo, ni kuwajengea uwezo waandishi wa mikoa hiyo waweze kuandika habari za misitu ili kusaidia kuibua mijadala ambayo itaiwezesha serikali, kutatua kero ambazo zimekuwa zikijitokeza juu ya uvunaji haramu wa misitu.


Alisema waandishi wa habari wanapaswa kuisaidia jamii na wadau wa misitu ili kuweza kuilinda, kutokana na kuwepo kwa changamoto kubwa katika kuilinda kutotekelezwa ipasavyo.

Awali akifungua mafunzo hayo, Kaimu mkurugenzi wa Halmashauri ya Lindi Suleiman Ngaweje aliwataka waandishi wa habari kutumia mafunzo watakayopata kutoa taarifa mbalimbali za misitu kwa wananchi, ikiwemo pia matumizi endelevu ya misitu ili wananchi waweze kunufaika nayo.


“Waandishi wa habari nawaomba mkawe mabalozi wazuri kwa kuwaeleza wananchi manufaa ya misitu na matumizi endelevu, misitu ni mali yetu tuitunze ili iweze kutusaidia kupata kipato na kukuza maendeleo yetu”, alisema Ngaweje.

No comments: