Tuesday, July 7, 2015

NYASA WAMPATA MRITHI WA KAPTENI KOMBA MJUMBE WA NEC


Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma, wakishangilia kwa pamoja kumpata mjumbe wa NEC wa wilaya hiyo Alex Shauri, mara baada ya uchaguzi kufanyika jana wilayani humo. (Picha na Kassian Nyandindi)
Na Kassian Nyandindi,
Nyasa.

WANACHAMA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Nyasa mkoa wa Ruvuma, wametakiwa kuwa makini kwa kutokubali kutumiwa na wagombea wanaowania nafasi ya ubunge wilayani humo hasa kwa wale ambao wamekuwa na tamaa ya madaraka, badala yake jukumu lao kubwa ni kuwachuja ili kuona kama kweli watakuwa na uwezo na moyo wa kuwasaidia wananchi, pale watakapokuwa wamepewa nafasi ya kuwaongoza.

Aidha wametakiwa kuhakikisha kwamba, CCM kinapata ushindi wa kishindo katika uchaguzi mkuu ujao unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25 mwaka huu, ambapo hilo litatokana na kujenga mshikamano wa dhati ikiwemo kutangaza kwa wananchi yale yote yaliyotekelezwa kwa vitendo na chama hicho, kama ilivyoainishwa ndani ya ilani yake ya uchaguzi.

Hayo yalisemwa na Mjumbe wa NEC wa wilaya ya Nyasa, Alex Shauri alipokuwa akiwashukuru wajumbe wenzake wa Chama Cha Mapinduzi wilayani humo, mara baada ya kumchagua kupeperusha bendera ya nafasi hiyo katika wilaya hiyo.


“Ndugu zangu mwaka huu tuwe waangalifu sana, tuchague viongozi bora kwenye kura za maoni katika chama chetu zinazotarajiwa kufanyika hivi karibuni, tuwe waaminifu tusichague kiongozi ambaye baadaye tutashindwa kumuuza kwa wananchi wakati uchaguzi mkuu utakapofanyika”, alisema Shauri. 

Uchaguzi wa kumpata mjumbe wa nafasi hiyo ulifanyika Julai 6 mwaka huu kwenye ukumbi wa Bay Live uliopo mjini hapa, ambapo kinyang’anyiro hicho kilikuwa na wagombea watatu ambao ni Ludwick Kumburu, Adam Mhaiki na Alex Shauri.

Shauri aliweza kushinda kwa kishindo kwa kuwagaragaza wenzake huku akiwaacha mbali kwa kupata kura 105, Kumburu alipata kura 16 na Mhaiki kura 6.

Awali akizungumza na wajumbe waliohudhuria katika uchaguzi huo mara baada ya kutangaza matokeo hayo msimamizi mkuu wa uchaguzi, Zainabu Chinoa ambaye pia ni Katibu wa CCM wilaya ya Mbinga mkoani hapa alisema vyama vya upinzani, siku zote vimekuwa na kawaida ya kuwarubuni wanachama wa chama hicho tawala kwa kuwadanganya wakiuke sheria za nchi, ikiwemo kuandamana bila kibali halali huku wao wenyewe wakirudi nyuma jambo ambalo mwisho wake husababisha kukumbana na matatizo makubwa, ikiwemo hata kupelekwa mahakamani.

Chinoa aliongeza kuwa wakati umefika sasa kwa wanachama wa chama hicho kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali za uongozi, lakini pia wahamasishe wale ambao sio wanachama wa CCM wajiunge ili kuongeza idadi ya wanachama.

Pamoja na mambo mengine, uchaguzi huo wa kumpata mjumbe wa NEC wilayani Nyasa ulifanyika kutokana na aliyekuwa katika nafasi hiyo, Kapteni John Komba kufariki dunia.

No comments: