Monday, July 20, 2015

MWANDISHI WA HABARI KASSIAN NYANDINDI ATANGAZA RASMI NIA YA KUGOMBEA UDIWANI KATA YA MBINGA MJINI A

Mwandishi wa habari Kassian Nyandindi, ambaye ametangaza nia ya kugombea udiwani katika kata ya Mbinga mjini A, iliyopo wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi. (CCM)
Na Dustan Ndunguru,
Mbinga.

KASSIAN Nyandindi ambaye amebobea katika fani ya uandishi wa habari, na sasa anaandikia gazeti la Majira mkoani Ruvuma, ametangaza nia yake ya kugombea udiwani katika kata ya Mbinga mjini A, iliyopo wilayani Mbinga mkoani humo kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Akizungumza leo na vyombo mbalimbali vya habari mjini hapa, Nyandindi alisema amekwisha chukua fomu ya kuwania nafasi hiyo na kuirejesha, huku akitamka vipaumbele vyake endapo wananchi wa kata hiyo watampatia ridhaa ya kuwaongoza, atahakikisha huduma muhimu za kijamii zinaboreshwa.

Alisema atazingatia kwamba miundombinu mbalimbali kama vile barabara za mitaa, afya, maji na elimu vinaboreshwa huku akisisitiza kuboresha elimu kutoka ngazi ya elimu ya msingi hadi sekondari kwa kuwataka pia wazazi kupeleka watoto wao shule na kuwapatia mahitaji muhimu ili mtoto aweze kusoma vizuri.  

“Uwezo wa kuongoza na kushughulikia matatizo ya wananchi wa kata hii ninao, kinachotakiwa hapa ni kutumia rasilimali tulizonazo ili tuweze kujipatia maendeleo na kuweza kuondokana na umasikini”, alisema Nyandindi.


Vilevile alieleza kuwa ili kuweza kuleta mafanikio katika hayo, atahitaji ushirikiano wa kutosha na usimamizi mzuri wa pamoja katika kusimamia maendeleo ya wananchi, ili kuleta ufanisi wenye tija katika jamii.

Alifafanua kuwa kutokana na taaluma yake aliyonayo ya uandishi wa habari, atawaunganisha akina mama, wazee na vijana kwa kuwapa mbinu za kuunda vikundi vya ujasiriamali ili baadaye waweze kukopesheka na taasisi za kifedha hatimaye waweze kusonga mbele, na kuepukana na tabia ya kuwa tegemezi.

“Katika safari hii ninaimani peke yangu siwezi kufika, lakini wanaccm wenzangu ninawaomba waniunge mkono ili niweze kuingia madarakani na kuleta mabadiliko ya kweli kwa kutekeleza mambo mbalimbali ya kimaendeleo, katika kata yangu ya Mbinga mjini A”, alisema.

Nyandindi anaongeza kuwa sababu kubwa iliyomsukuma kugombea nafasi hiyo, ilitokana na kuchoshwa na viongozi waliokuwepo madarakani kwa muda mrefu kutoa ahadi ambazo hawazitekelezi, na wananchi wakiendelea kuteseka.

Hata hivyo alibainisha kuwa wananchi wa kata hiyo wanachohitaji sasa ni kumpata kiongozi shupavu, mwenye kuweza kuleta mabadiliko ya kweli  na kuboresha maisha ya wananchi kwa kuzungumzia kero zao katika vikao mbalimbali na kuhakikisha zinatekelezwa ipasavyo.

No comments: