Monday, August 3, 2015

MATOKEO KURA ZA MAONI MBINGA UTATA MTUPU, HALI NI TETE WANACHAMA WAVAMIA ENEO LA OFISI ZA CCM WILAYA

Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

HALI ya kisiasa wilayani mbinga mkoa wa Ruvuma, si shwari au kwa maneno mengine imechafuka ambapo Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani humo, kimeingia katika hali tete kufuatia baadhi ya wanachama wa chama hicho wilayani humo, kuvamia katika eneo la ofisi za chama hicho na kuutaka uongozi wa CCM wilaya kutangaza matokeo ya uchaguzi kura za maoni kwa nafasi ya ubunge, kufuatia matokeo ya nafasi hiyo kukaa muda mrefu kwa siku mbili, bila kutangazwa.

Aidha kufuatia hali hiyo, Jeshi la Polisi wilayani humo limeonekana askari wake wakidhibiti hali hiyo huku wengine wakionekana kubeba silaha za moto, na mabomu ya machozi.

Baadhi ya wanachama wa chama hicho wameendelea kuandamana maeneo mbalimbali ya mji wa Mbinga, wakitishia kutoondoka katika maeneo ya ofisi za CCM na kuonekana kuranda randa wakitamka maneno…………….“hapa mpaka kieleweke, tunachotaka ni matokeo na sio vinginevyo”.

Hali hiyo imejitokeza leo kufuatia kutotangazwa kwa matokeo ya kura za maoni ya chama hicho tawala kwa muda wa siku tatu sasa, ambao umefanyika mapema Agosti Mosi mwaka huu, kwa jimbo la Mbinga mjini na Mbinga vijijini.


Duru za siasa mjini hapa kutoka makao makuu ya Ofisi za CCM wilayani humo, zinasema katika majimbo hayo Mbinga mjini mpaka sasa linadaiwa kuongozwa kwa kura za maoni na Sixtus Mapunda, kati ya wagombea watatu waliokuwa wakiwania nafasi hiyo na vijijini, Martin Msuha ambaye naye alikuwa akishindana na wagombea wenzake nane.

Sinto fahamu inaendelea kutawala katika eneo la ofisi za CCM wilaya ya Mbinga, na kutishia muendelezo wa amani katika eneo la ofisi hizo, ambapo wanachama wa chama hicho wanaonekana kujawa jazba na kuutaka uongozi husika utangaze matokeo ya nafasi hiyo ya ubunge, kutokana kucheleweshwa kutangazwa.

“Tunataka matokeo, tunataka matokeo, tunataka matokeo hapa mkitaka amani tuleeteeni matokeo vinginevyo tunarudisha kadi za CCM hatukitaki chama tunataka haki itendeke kwa mshindi aliyeshinda”, hayo ni maneno ambayo yalikuwa yakitawala katika eneo la ofisi kuu za chama hicho wilayani humo.

Kadhalika licha ya Katibu wa Chama Cha Mapinduzi mkoa wa Ruvuma, Verena Shumbusho kujitokeza mbele ya hadhira ambayo ilionekana kudai matokeo hayo katika viwanja vya chama hicho, bado wanachama walionekana kujawa jazba wakitamka maneno ya kutaka matokeo yatangazwe na wengine wakiendelea kutamka maneno hawawezi kuondoka mpaka kieleweke.

“Ndugu zangu tulizeni jazba, lazima tufuate utaratibu wa chama, hatuwezi kuendesha chama kwa mashinikizo”, alisikika akisema Shumbusho mbele ya umati huo uliokuwa kwenye viwanja vya CCM mjini hapa.

Baadhi ya wanachama wa chama hicho waliendelea wakisema, wanamashaka na viongozi wa wilaya hiyo wakiwemo chama na serikali, huenda wanapanga mpango wa kutaka kuyachakachua matokeo ili atangazwe mgombea ambaye sio chaguo sahihi la wananchi.

Mpaka sasa habari hizi zinaingia katika mtandao huu, hali ni tete katika eneo la ofisi za CCM wilayani Mbinga, kutokana na umati mkubwa wa watu ukiendelea kutawala katika eneo hilo huku askari polisi wakiendelea kuimarisha ulinzi na kutaka matokeo yatangazwe haraka, kutokana na kucheleweshwa kutangazwa.

Waandishi wa habari ambao walikuwa wakishuhudia juu ya sakata hilo na kumtaka Katibu wa wilaya hiyo, Zainabu Chinowa azungumzie juu ya hali hiyo alisema kuwa mpaka sasa wanashindwa kutangaza matokeo kutokana na baadhi ya vituo viwili vya jimbo la Mbinga mjini, kesho Agosti 4 mwaka huu wanachama wa CCM wanalazimika kurudia kupiga kura kwa nafasi ya udiwani na jimbo la vijijini katika kata ya Kihangimahuka, kuwepo kwa utata juu ya matokeo ya nafasi ya ubunge.

“Chama kimetuma magari huko Kihangimahuka kufuatilia juu ya suala hili, kwa sababu matokeo yanaleta utata kidogo, hivyo yakiletwa na chama kujiridhisha juu ya jambo hili kesho mapema asubuhi majira ya saa mbili hadi saa tatu tutangaza matokeo, naomba wananchi waache jazba wakati tunaendelea na mchakato huu”, alisema Chinowa.

No comments: