Friday, August 28, 2015

KAPINGA KUWALETEA NEEMA WANANDILIMALITEMBO SONGEA

Cresensia Kapinga.
Na Mwandishi wetu,
Songea.

CRESENSIA Kapinga ambaye ni mgombea udiwani kata ya Ndilimalitembo, Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) amesema atatumia nafasi hiyo ya uongozi mara baada ya kuingia madarakani, kwa kuwatumikia wananchi ipasavyo wa kata hiyo hasa katika suala zima la kusukuma mbele maendeleo yao kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Aidha Kapinga amewashukuru wanachama wa CCM ndani ya kata hiyo, kwa maamuzi yao ya kumpatia heshima ya kugombea udiwani licha ya kukiri kwamba mchakato wa kura za maoni kwa tiketi ya chama hicho ulikuwa mgumu, hivyo atakapotimiza ndoto yake mara baada ya kuchaguliwa na wananchi katika uchaguzi mkuu Oktoba 25 mwaka huu, ataendeleza ushirikiano na wananchi wake katika kutekeleza yale yaliyopo kwenye ilani ya Chama Cha Mapinduzi.

“Endapo nitashinda kwenye kinyang’anyiro hiki cha uchaguzi mkuu wa mwezi Oktoba mwaka huu, kubwa nitakalolifanya ni kutekeleza ilani ya chama changu ili niweze kuwaletea wananchi wangu maendeleo kwa haraka zaidi”, alisema Kapinga.


Alifafanua kuwa katika kutimiza majukumu husika na kuweza kuleta ufanisi mzuri wa kimaendeleo, atahakikisha pia anatoa fursa sawa kwa makundi yote ya kijamii ili kuweza kuleta mabadiliko ya kweli katika jamii.

Kapinga alisema hayo alipokuwa akihojiwa na vyombo mbalimbali vya habari mjini Songea, huku akiongeza kuwa kwa mara ya kwanza aligombea udiwani wa viti maalum mwaka 2010 kupitia CCM ambapo kura hazikutosha lakini mwaka huu ameweza kujaribu tena na kufanikiwa kupitia chama hicho na kuwa mgombea udiwani wa kata ya Ndilimalitembo, kwa kuwabwaga chini wagombea wenzake watatu ambao waliingia kwenye kinyang’anyiro hicho kupitia kura za maoni.
 

No comments: