Tuesday, August 4, 2015

MATOKEO UCHAGUZI KURA ZA MAONI NAFASI YA UBUNGE MBINGA VIJIJINI MARTIN MSUHA AIBUKA KIDEDEA

Kushoto ni Martin Msuha siku alipokuwa akichukua fomu ya kugombea nafasi ya ubunge kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwenye ofisi ya chama hicho wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma. Anayemkabidhi fomu hiyo ni Katibu msaidizi wa chama hicho ndugu Mrope.
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

KUFUATIA vuguvugu la kisiasa ambalo limeendelea kushika kasi na kutishia hali ya amani katika ofisi za Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, kutokana na wananchi kuutaka uongozi husika wa chama hicho wilayani humo utangaze matokeo ya nafasi ya ubunge, hatimaye matokeo hayo yalitangazwa kwa jimbo la Mbinga vijijini majira ya saa 5:45 usiku.

Kabla ya kutangazwa kwa matokeo hayo kwa jimbo hilo, kulikuwa na mvutano mkali ambao ulidumu kwa masaa 12, kutokana na kati ya wagombea nane waliokuwa katika kinyang’anyiro hicho, mgombea Gaudence Kayombo kudaiwa kufanya mchezo mchafu wa kutaka kuchakachua matokeo kwa kata ya Ruanda na Kihangimahuka, ili yaweze kumpatia ushindi baada ya kuona hali ya upepo wa ushindi kwa upande wake inamwendea vibaya.

Aidha kufuatia hali hiyo, Jeshi la Polisi wilayani humo lililazimika askari wake kuweka ulinzi mkali katika eneo la ofisi hizo za CCM, kutokana na baadhi ya wanachama kuleta vurugu huku wengine wakirusha mawe.


Baadhi ya wanachama wa chama hicho waliendelea kuandamana maeneo mbalimbali ya mji wa Mbinga, wakitishia kutoondoka katika maeneo ya ofisi za CCM na kuonekana kuranda randa huku wakiimba nyimbo mbalimbali na kutamka maneno…………….“hapa mpaka kieleweke, tunachotaka ni matokeo na sio vinginevyo”.

Sinto fahamu iliendelea kutawala katika eneo la ofisi za CCM wilaya ya Mbinga ambapo wanachama wa chama hicho walionekana kuendelea kujawa jazba na kuutaka uongozi husika utangaze matokeo ya nafasi hiyo ya ubunge, kutokana kucheleweshwa kutangazwa.

“Tunataka matokeo, tunataka matokeo, tunataka matokeo hapa mkitaka amani tuleeteeni matokeo vinginevyo tunarudisha kadi za CCM hatukitaki chama tunataka haki itendeke kwa mshindi aliyeshinda”, hayo ni maneno ambayo yalikuwa yakitawala katika eneo la ofisi kuu za chama hicho wilayani humo ambayo yalikuwa yakitamkwa na wanachama wa chama hicho.

Kadhalika licha ya Katibu wa Chama Cha Mapinduzi mkoa wa Ruvuma, Verena Shumbusho kujitokeza mbele ya hadhira hiyo ambayo ilionekana kudai matokeo hayo katika viwanja vya chama hicho, bado wanachama walionekana kujawa jazba wakitamka maneno ya kutaka matokeo yatangazwe na wengine wakiendelea kutamka hawawezi kuondoka mpaka kieleweke.

“Ndugu zangu tulizeni jazba, lazima tufuate utaratibu wa chama, hatuwezi kuendesha chama kwa mashinikizo”, alisikika akisema Shumbusho mbele ya umati huo uliokuwa kwenye viwanja vya CCM mjini hapa.

Baadhi ya wanachama waliendelea wakisema, wanamashaka na viongozi wa wilaya hiyo wakiwemo chama na serikali, huenda wanapanga mpango wa kutaka kuyachakachua matokeo ili atangazwe mgombea ambaye sio chaguo sahihi la wananchi.

Waandishi wa habari ambao walikuwa wakishuhudia juu ya sakata hilo na kumtaka Katibu wa wilaya hiyo, Zainabu Chinowa azungumzie juu ya hali hiyo alisema kuwa mpaka sasa wanashindwa kutangaza matokeo kutokana na jimbo hilo la Mbinga vijijini katika kata ya Ruanda na Kihangimahuka, kuwepo kwa utata juu ya matokeo ya nafasi ya ubunge.

“Ndugu zangu waandishi wa habari chama kimetuma magari huko Kihangimahuka na Ruanda kufuatilia juu ya suala hili, kwa sababu matokeo yanaleta utata kidogo, hivyo yakiletwa na chama kujiridhisha juu ya jambo hili tutayatangaza muda wowote hata kama itakuwa ni usiku nawaomba wananchi waache jazba wakati tunaendelea na mchakato huu”, alisema Chinowa.

Kadhalika baada ya kukamilika kwa taratibu husika za chama ndipo matokeo kwa nafasi ya ubunge wa jimbo la Mbinga vijijini yalitangazwa Agosti 3 mwaka huu majira ya saa 5:45 usiku ambapo, Martin Msuha aliweza kuchukua nafasi ya ushindi katika jimbo hilo kwa kupata kura 13,354 na kuwagaragaza chini wagombea wenzake saba, waliokuwepo kwenye kinyang’anyiro hicho.

Wagombea wengine waliokuwa wakiwania nafasi hiyo na kura walizopata katika mabano kuwa ni; Humprey Kisika (545), Dokta Silverius Komba (1,289), Edesius Kinunda (2,355), Deodatus Mapunda (2,532), Benaya Kapinga (3,941), Deodatus Ndunguru (7,060) na Gaudence Kayombo aliyepata kura 12,068.

Pamoja na mambo mengine, wilaya ya Mbinga ambayo ina majimbo mawili ya uchaguzi Mbinga mjini na vijijini ambapo kwa upande wa jimbo hilo la mjini matokeo yake kwa nafasi ya ubunge yanatarajiwa kutangazwa leo majira ya jioni, baada ya kumalizika kwa uchaguzi mdogo ambao unaendelea katika kata ya Kikolo na Uzena zilizopo wilayani humo.

No comments: