Wednesday, August 12, 2015

KATIBU CCM NYASA AENDELEA KUSHUSHIWA LAWAMA

Na Muhidin Amri,
Nyasa.

MAKADA tisa kati ya kumi kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma, ambao waliangukia pua katika mchakato wa kura za maoni kuomba ridhaa ya kugombea nafasi ya ubunge jimbo la Nyasa, wamemnyoshea kidole katibu wa chama hicho wilayani humo Grayson Mwengu, kuwa ndiye aliyechangia wao kushindwa vibaya katika mchakato huo.

Wanachama waliogombea nafasi hiyo na kushindwa kuwa ni Christopher Challe, Ebehard Haule, Adolph Kumburu, Dokta Stephen Maluka, Frank Mvunjapori, Alex Shauri, Gerome Mathayo, Cassian Njowoka na Oddo Mwisho walisema katibu huyo wa chama alikuwa akimpendelea mgombea mwenzao Stella Manyanya ambaye aliwashinda kwa idadi kubwa ya kura.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na mwandishi wetu; Alex Shauri, Christopher Challe na Stephen Maluka walisema kuwa katibu huyo wa chama wilaya hakuweza kutoa ushirikiano kwao, badala yake alikuwa akimkumbatia mgombea mmoja na kuwasusa wengine.


Walisema kutokana na hali hiyo kuna uwezekano mkubwa kwa CCM kutofanya vizuri katika uchaguzi mkuu ujao jimbo la Nyasa, kwa nafasi ya udiwani na ubunge kwa madai kuwa baadhi ya wanachama tayari wameonesha kukata tamaa juu ya mwenendo wa utendaji kazi, wa katibu huyo.

“Mimi nina imani kama hakutafanyika mabadiliko ya kumuondoa katibu huyu wa chama wilaya, basi hatuwezi kupata ushindi katika jimbo hili la Nyasa wanachama wamekatishwa tamaa na uongozi wa chama wilaya kwani kila tunapofika ofisini kwake ni mtu mwenye dharau na kiburi, hataki kutupatia ushirikiano”, alisema Shauri.

Shauri ambaye pia ni mjumbe wa Halmashauri kuu (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi wilaya ya Nyasa, ameuomba uongozi husika wa chama kuangalia uwezekano wa kumwajibisha Mwengu kwani anaweza kusababisha chama kikashindwa vibaya, katika uchaguzi mkuu ujao wilayani humo.

Naye Christopher Challe alisema tangu katibu huyo alipoletwa na chama wilayani humo amekuwa ni mtu mwenye kujenga makundi, ambayo yanahatarisha kukua kwa maendeleo ya chama.


Kwa upande wake Katibu wa CCM wilaya ya Nyasa, Mwengu alipofuatwa ili aweze kutoa ufafanuzi juu ya madai hayo alikataa kuzungumza huku akisema kwamba, hana muda wa kuweza kuzungumza na waandishi wa habari.

No comments: