Wednesday, August 12, 2015

VITA KAWAWA AGARAGAZWA CHINI BAADA YA UCHAGUZI KURUDIWA

Na Mwandishi wetu,
Namtumbo.

HATIMAYE mchakato wa kura za maoni kuwapata wagombea nafasi ya ubunge katika majimbo mawili ya Tunduru kaskazini na Namtumbo hapa mkoani Ruvuma, ambapo majimbo hayo yalichelewa kukamilisha mchakato huo kutokana na sababu mbalimbali, hivyo ulifanyika tena mwishoni mwa wiki na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwachagua Mhandisi Ramo Makani kuwa mgombea kwa jimbo la Tunduru kaskazini na Edwin Ngonyani jimbo la Namtumbo.

Mchakato haukukamilika kwa muda uliopangwa kutokana na kujitokeza kwa baadhi ya kasoro, ambazo zilisababisha wanachama walioshiriki kugombea nafasi hiyo kugomea matokeo husika kwa madai kwamba walichezewa rafu na wagombea wenzao.

Jimbo la Namtumbo uchaguzi kura za maoni ulilazimika kurudiwa kutokana na kuwepo kwa madai ya idadi kubwa ya kura zilizopigwa, tofauti na wanachama halisi waliostahili kupiga kura kitendo ambacho kililalamikiwa na wagombea wengine waliokuwemo kwenye mchakato huo.


Wagombea hao waligomea matokeo yaliyomtangaza Vita Kawawa kuwa ni mshindi, ambapo kwa mujibu wa Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Namtumbo Aziz Fikiri alisema kutokana na kuwepo kwa malalamiko hayo Katibu mkuu Taifa CCM, Abdulharman Kinana aliagiza kurudiwa kwa uchaguzi huo.

Agizo hilo lilionekana kuwa chungu kwa mshindi huyo wa matokeo ya kwanza, ambaye naye alisusia kushiriki katika marudio ya uchaguzi huo ambao ulifanyika kwenye baadhi ya maeneo, ambayo ni ngome kwa wagombea wengine na maeneo ambayo Kawawa anakubalika, wapiga kura walikataa kurudia kupiga kura.

Mbali na kususia kwa uchaguzi huo, Kawawa hakuweza hata kuonekana ndani ya maeneo ya wilaya hiyo wakati uchaguzi ulipokuwa ukifanyika.

Pamoja na mambo mengine, jimbo la Tunduru Kaskazini uchaguzi ulichelewa kufanyika kwa muda wa siku tatu kufuatia wagombea watano kati ya sita ambao walishiriki katika kinyang’anyiro hicho cha kuomba ridhaa kwa tiketi ya CCM kugombea nafasi ya ubunge katika jimbo hilo, walimkataa katibu wa chama hicho wilaya ya Tunduru, Mohamed Lawa kwa madai kuwa alikuwa akimbeba mgombea Ramo Makani ili aweze kurudi tena kwenye nafasi yake ya ubunge.


Hata hivyo katika uchaguzi huo wanachama wa chama hicho kwenye jimbo hilo waliweza kumchagua tena Makani, kugombea ubunge jimbo la Tunduru kaskazini baada ya kuwashinda wagombea wenzake.

No comments: