Friday, August 7, 2015

MWAMBUNGU AWAPA SOMO WANACCM RUVUMA

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu.
Na Mwandishi wetu,
Songea.

WANACHAMA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Ruvuma, wametakiwa kuwa na upendo, umoja na ushirikiano katika maisha yao ya kila siku jambo ambalo litasaidia chama kupata ushindi wa kishindo katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu.

Aidha wamekumbushwa kuacha tabia ya kukatishana tamaa, kwani hali hiyo inaweza kuwaamsha wapinzani wao kutoka kwenye vyama mbalimbali vya kisiasa waweze kujipanga vizuri na kuleta ushindani mkubwa, kwa wagombea wa Chama Cha Mapinduzi.

Rai hiyo ilitolewa na MKuu wa mkoa huo, Said Mwambungu alipokuwa akizungumza na wanawake wa CCM kwenye mkutano mkuu wa uchaguzi wa wabunge wa viti maalum, uliofanyika ukumbi wa Parokia ya Mtakatifu Theresia Bombambili mjini Songea.


Mwambungu alisema chama hicho ni taasisi kubwa ambayo haimtegemei mtu mmoja katika uendeshaji wa shughuli zake za kichama, hivyo si jambo jema kuona mwanachama anajivua uanachama wake kwa sababu tu ya kushindwa kwa mgombea ambaye alikuwa akimpigia kampeni, ili aweze kushinda katika nafasi aliyoitaka.

Mkuu huyo wa mkoa amewahimiza wanaccm mkoani humo, kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo, ili kuwavutia watu wengine ambao wanaweza kuhamasika na kujiunga na chama hicho.

“Ninyi mliopo hapa ni sehemu ya jamii huko muendako mkashiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya wananchi, kufanya hivi mtaweza kukifanya chama kuwa na wanachama wapya wengi zaidi”, alisema Mwambungu.

Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa mkoa wa Ruvuma, alisema kuwa upendo, umoja na mshikamano ndiyo silaha pekee itakayokiwezesha Chama Cha Mapinduzi kupendwa, kuungwa mkono na watu wengine zaidi.



No comments: