Tuesday, August 18, 2015

WANANCHI WATAKIWA KUPEWA ELIMU SAHIHI UTUNZAJI WA MISITU

Na Steven Augustino,
Masasi.

UKOSEFU wa ushirikishwaji na utoaji wa elimu ya kutosha juu ya uhifadhi shirikishi wa misitu ndiyo chanzo cha jamii, kuendelea kufanya shughuli za uvunaji holela wa mazao ya misitu.

Kutokana na hali hiyo, wananchi wa kijiji cha Ulungu kata ya Sindano wilayani Masasi mkoa wa Mtwara wameamua kufunga kwa muda usiofahamika ufanyaji wa shughuli zote za uvunaji mazao ya misitu, hadi pale watakapojiridhisha na maendeleo ya uoto wa asili katika msitu wa kijiji hicho.

Wananchi hao walibainisha hayo walipokuwa wakizungumza na waandishi wa habari, ambao walitembelea kijijini hapo kutaka kujua mgawanyo wa mamlaka na majukumu katika usimamizi wa misitu kati ya Meneja wa misitu wa wilaya (TFS) na Afisa misitu wilaya (DFO) pamoja na kamati za maliasili za vijiji.


Kwa nyakati tofauti wakizungumza kwa niaba ya wananchi wa kijiji hicho, Victor Athuman, Mathayo Patrick, Ahamad Machopa na mwakilishi wa waganga wa tiba za asili kijijini hapo, Rukia Abdalah walisema pamoja na kuundwa kwa kamati za maliasili lakini bado haijatolewa elimu ya kutosha kwa wananchi juu ya umuhimu wa utunzaji shirikishi wa misitu.

“Pamoja na kuwepo kwa kamati zinazosimamia utunzaji wa misitu, lakini bado wananchi wa kijiji chetu hatuna elimu ya kutosha kuhusu utunzaji wa misitu”, alisema Bi. Rukia.

Mwananchi mwingine aliyezungumzia matukio hayo, Victor Athuman ambaye pamoja na mambo mengine alidai kuwa vitendo hivyo vimekuwa vikichangiwa na umasikini mkubwa walionao wananchi wa kijiji cha Ulungu.

“Tatizo kubwa lililopo kwa wananchi wa kijiji hiki na hadi tunafikia hatua ya kushambulia msitu tulionao, ni kutokana umaskini tulionao tunakata miti ili tuweze kupata mbao tukaziuze tupate fedha, tunachoma mkaa na matumizi mengine ili tuweze kuingiza kipato cha kuendeshea familia zetu”, alisema Athuman.

Walisema bado elimu ya uhifadhi wa misitu ngazi ya vijiji haijatolewa ipasavyo, jambo ambalo wananchi kwenye maeneo yao wamekuwa chanzo kikubwa katika uharibifu wa rasilimali hiyo muhimu.

Ofisa maliasili wa Halmashauri ya wilaya ya Masasi, Gabriel Joshua licha ya kutolewa elimu kwa wananchi wa maeneo ya utunzaji na uhifadhi shirikishi wa misitu, wananchi wamekuwa wagumu kupokea elimu husika.


“Tunajitahidi sana kutoa elimu kwa wananchi wetu pamoja na kamati za maliasili za vijiji, lakini jamiibado haipokei  elimuhiyo na badala yake wamekuwa wakiendeleza vitendo vya uharibifu ikiwemo uvunaji holela wa misitu”, alisema Joshua.

No comments: