Thursday, August 27, 2015

WANAFUNZI NAMTUMBO WATAKIWA KUONGEZA JUHUDI KATIKA MASOMO YAO

Na Mwandishi wetu,
Namtumbo.

MWITO umetolewa kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma, kuongeza juhudi katika masomo yao na kujiepusha kushiriki vitendo viovu vinavyoweza kukatisha ndoto yao ya kujiendeleza kimasomo kama vile kwa wanafunzi wa kike kupata mimba wakati wakiwa na umri mdogo, au virusi vya Ukimwi.

Aidha wametakiwa kuwa na dhamira ya kweli juu ya kusukuma maendeleo ndani ya wilaya yao, ili watakapohitimu masomo yao na kupata ajira warudi kwenye maeneo yao kuwatumikia wananchi na sio kwenda kufanya kazi katika mikoa au wilaya zingine ambako tayari wamepiga hatua kimaendeleo.

Imeelezwa kuwa kufanya hivyo kutasaidia kupunguza tatizo la watumishi, hasa kwa idara ya afya, elimu na kilimo ambako mahitaji ya watumishi wake ni makubwa.


Tekra Nyoni ambaye ni Afisa mipango wilaya ya Namtumbo, alisema hayo kwa nyakati tofauti alipokuwa akikagua ujenzi wa vyumba vya maabara shule ya sekondari Chengena na Luchili wilayani humo, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais Jakaya Kikwete la kutaka kila shule ya sekondari hapa nchini kuwa na vyumba vitatu vya maabara, kwa lengo la kutoa fursa kwa wanafunzi wa shule hizo kusoma masomo ya sayansi kwa urahisi.

Kwa mujibu wa Nyoni, alisema kuwa wilaya hiyo inakabiliwa na upungufu mkubwa wa vyumba vya maabara na watumishi katika sekta hiyo ya elimu.


Afisa mipango huyo amewataka wanafunzi wa kike kuwa na moyo wa uvumilivu ikiwemo kukataa kurubuniwa na wanaume wenye tamaa ya ngono, ili waweze kuepukana na kupata mimba zitakazosababisha kukatisha masomo yao na badala yake muda mwingi wajikite katika masomo yao darasani.

No comments: