Saturday, August 29, 2015

SERIKALI YAPONGEZWA KWA KUTAMBUA MCHANGO WA KUINUA TAALUMA TUNDURU

Mkuu wa shule ya sekondari Frankweston mwalimu Hassan Mussa, akionesha cheti cha pongeza kwa baadhi ya walimu walioshiriki katika hafla hiyo.
Na Mwandishi wetu,
Tunduru.

WALIMU wanaofundisha katika shule za sekondari wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, wameipongeza serikali kwa kujali na kutambua mchango wao katika kuinua elimu ambapo wilaya hiyo, ilianza kuporomoka.

Kwa nyakati tofauti walimu hao walitoa pongezi hizo, walipokuwa wakipokea vyeti vyao vya pongezi kutokana na shule zao kufanya vizuri katika matokeo ya mtihani wa kidato cha nne, mwaka 2014.

Mkuu wa shule ya sekondari Frankweston Hassan Mussa, George Martin wa Mataka Sekondari na Elis Banda wa shule ya wasichana Masonya wilayani humo walieleza kuwa kitendo cha serikali kuwapatia vyeti hivyo, kimeonesha kujali ukuzaji wa taaluma na ujuzi ambao walimu wamekuwa wakiutoa kwa wanafunzi wao.


Awali Afisa elimu wa shule za sekondari wa wilaya ya Tunduru, Ally Mtamila na Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Tina Sekambo walisema pamoja na utoaji wa vyeti hivyo pia wameweza kuwapatia walimu hao motisha ya fedha na kuwaandikia barua za kuwapongeza, juu ya jitihada hizo walizozifanya na kuweza kuzaa matunda hayo na kwamba mpango huo unatekelezwa na serikali kupitia mpango wake wa matokeo makubwa sasa (BRN).

Kadhalika Afisa elimu huyo alitumia nafasi hiyo kuwaasa walimu wake wilayani humo, kutobweteka na sifa hizo badala yake waongeze juhudi na kuzifanya shule hizo kuendelea kufanya vizuri katika matokeo yajayo.

Alifafanua kwamba katika matokeo hayo shule ya sekondari Masonya, shule za kutwa za Frankweston na Mataka ndizo zilizotuzwa vyeti hivyo vya pongezi na Waziri wa elimu na mafunzo ya ufundi, Shukuru Kawambwa.

Katika matokeo hayo Masonya ilifanya vizuri baada ya kushika nafasi ya kwanza kiwilaya kati ya shule 19, nafasi ya 20 kimkoa kati ya shule 63, ya 138 kikanda kati ya shule 395 na kushika nafasi ya 945 kitaifa kati ya shule 2,322.

Vilevile shule ya Frankweston nayo imepata pongezi hizo, kutokana na kushika nafsi ya 4 kiwilaya kati ya shule 19, ya 52 kimkoa kati ya shule 63, ya 351kikanda kati ya shule 395 na nafasi ya 2,144 kitaifa kati ya shule 2,322 ambazo zilifanya mtihani huo hapa nchini.

Mwalimu Mtamila alidai kwamba, upande wa shule za sekondari mbili zilizofanya vibaya katika matokeo hayo idara yake imezipatia barua ya onyo na kuwataka walimu wake kuzinduka kutoka usingizini, ikiwemo kuongeza juhudi katika kuinua taaluma kwa wanafunzi wao.

Alisema sambamba na maelezo ya jumla yaliyopo kwenye barua hizo, pia kuna kipengele kinachowataka wakuu wa shule hizo kuwajibika ikibidi kuachia madaraka waliyonayo, endapo shule zao zitaendelea kufanya vibaya katika matokeo ya mwaka huu 2015.


Hata hivyo amezitaja shule hizo kuwa ni; Mchoteka sekondari ambayo ilishika nafasi ya mwisho kiwilaya, mkoa na kitaifa ikiwa ni ya 2,309 kati ya shule 2,322, Mgomba sekondari ilishika nafasi ya 18 kati ya shule 19 zilizopo wilayani humo ya 61 kati ya 63 za mkoa ya 382 kikanda kati ya shule 395 na ya 2,292 kati ya 2,322 kitaifa.

No comments: