Friday, August 28, 2015

MANISPAA YA SONGEA YAPATA FEDHA ZA KUWAJENGEA UWEZO WANAOISHI KATIKA MAZINGIRA MAGUMU

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu.
Na Muhidin Amri,
Songea.

HALMASHAURI ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, imepokea kiasi cha shilingi milioni 345,213,000 kwa ajili ya kuwajengea uwezo watu wanaoishi katika mazingira magumu na kuziwezesha kaya maskini kuongeza kipato, ili waweze kuwa na uwezo wa kugharimia mahitaji yao muhimu katika maisha yao.

Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Nachoa Zakaria alisema hayo alipokuwa akizindua zoezi la malipo kwa walengwa wa mpango wa kunusuru kaya maskini, kutoka mitaa mitatu ya kata ya Ruvuma wilaya ya Songea ambao unatekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) awamu ya tatu, uliozinduliwa na Rais Jakaya Kikwete mapema mwaka huu.

Nachoa alifafanua kuwa kati ya fedha hizo, shilingi milioni 306,856,000 ni fedha za walengwa wenyewe, shilingi milioni 5,230,000 ambayo ni sawa na asilimia 1.5 ni fedha zitakazokwenda ngazi ya mitaa kwa ajili ya shughuli za usimamizi.


Kiasi cha shilingi milioni 3,477,000 zitatumika kwa ajili ya usimamizi ngazi ya kata na shilingi milioni 29,639,500 zitatumika katika ngazi ya halmashauri kwa ajili ya kazi kama hiyo ya ufuatiliaji na usimamizi, ambapo tayari kaya 7,915 kutoka mitaa 53 zinaendelea kulipwa.

Awali mratibu wa TASAF katika Manispaa hiyo, Christopher Ngonyani alisema kuwa ilikadiriwa kutambua kaya maskini 8,028 kutoka kwenye mitaa hiyo baada ya kufanyika upembuzi wa kina, kaya zilizoibuliwa na kukidhi vigezo zimefikia 7,915.

Ngonyani alisema fedha hizo zitatolewa kila baada ya miezi miwili na mpango huo ni wa muda wa miaka mitatu, ambapo wanufaika amewataka hasa akina mama kutumia fedha hizo kwa malengo yaliyokusudiwa.


Mratibu huyo ameshauri pia kutumia fedha hizo wanazozipata, kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ili ziwasaidie kupunguza gharama kubwa ya matibabu, pale wanapougua.

No comments: