Saturday, August 15, 2015

TASAF TUNDURU YAWANOA WATAALAMU WA KUNUSURU KAYA MASKINI

Na Mwandishi wetu,
Tunduru.

HALMASHAURI ya wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, imewaasa washiriki wa mafunzo ya uibuaji miradi kwa jamii kuwa wasikivu ili waweze kwenda kutoa ushirikiano katika hatua zote zitakazotakiwa kutekelezwa wakati wa utambuzi wa matatizo ya wananchi vijijini, hususani kwa yale yatakayolenga kuinua kipato katika jamii.

Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Tina Sekambo alisema hayo alipokuwa akifungua mafunzo ya siku saba kwa wataalamu 26 kutoka ngazi ya kata wilayani humo wanaojengewa uwezo, kuhusu utaratibu wa kutekeleza miradi ya kutoa ajira kwa muda ambayo inatekelezwa chini ya mpango wa kunusuru kaya maskini unaotekelezwa na TASAF awamu ya tatu.

Sekambo alifafanua kuwa baada ya wataalamu hao kukamilisha mafunzo hayo, watakwenda kuungana na wenzao 46 vijijini kwa ajili ya kubaini fursa na kuibua miradi itakayotoa ajira za muda, hasa kwa uboreshaji wa mindombinu kwenye maeneo yao huku walengwa hao wakinufaika kwa kuongeza kipato chao.


Sambamba na maelekezo hayo Mkurugenzi huyo aliwataka wataalamu hao kuzingatia, kuuliza, kusoma na kuwa wazi kwa mambo ambayo hawatakuwa wanayaelewa ili kuwawezesha kujengewa uelewa, utakaowafanya waende kutekeleza kazi hizo kwa weledi mkubwa.

Awali akisoma hotuba ya Mkurugenzi wa TASAF nchini, Ladslaus Mwamanga Meneja miradi ya kutoa ajira ya muda kwa walengwa, Barnabas Jachi alisema dhima kubwa ya uibuaji wa miradi hiyo inalenga kuimarisha miundombinu ya uhifadhi wa udongo, uvunaji maji, kudhibiti makorongo na kuotesha vitalu vya miti.

Jachi alifafanua kuwa mpango huo unafuatia uzinduzi wa mradi uliofanywa na Rais Jakaya Kikwete, Agosti 15 mwaka 2012 na kuanza kutekelezwa Februari mwaka 2013 ukiwa unalenga kunusuru kaya masikini.

Alisema kuwa baada ya mafunzo hayo washiriki hao watatakiwa kuja na mikakati ya pamoja ambayo watakwenda kuelimisha jamii, ambapo malengo na manufaa ya mpango huo ni kupunguza umasikini kwa wananchi waishio vijijini.


Pamoja na mambo mengine akizungumza kwa niaba ya washiriki wenzake Mwenyekiti wa mafunzo hayo, Omary Makina aliwatoa mashaka viongozi hao kwamba huko waendako watatekeleza wajibu wao kwa moyo na kujituma kwa nguvu zote, ili kuwawezesha wananchi waweze kufikia malengo yaliyowekwa na serikali kupitia mpango huo.

No comments: