Monday, August 10, 2015

CCM MBINGA YAMEGUKA BAADHI YA WENYEVITI WAKE WAHAMIA CHADEMA

Wenyeviti wawili wa vitongoji, Steven Mateso wa Mbinga mjini A akiwa na mwenzake wa kutoka kata ya Masumuni wakiwa pamoja kwenye mkutano wa hadhara wa CHADEMA wakati waliporudisha kadi za CCM na kujiunga na chama hicho, kwenye eneo la viwanja vya soko kuu mjini hapa. 

Wananchi waliohudhuria mkutano wa CHADEMA Mbinga mjini eneo la soko kuu, wakiwa na mabango yenye ujumbe wa aina mbalimbali.
Na Mwandishi wetu,
Mbinga.

CHAMA Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, kimesema kitaendelea kujenga misingi ya kutetea na kupigania haki na maendeleo ya wananchi wa wilaya hiyo, ili waweze kusonga mbele katika nyanja mbalimbali za kimaendeleo na hatimaye waondokane na umasikini.

Aidha chama hicho kimeeleza kuwa, katika uchaguzi mkuu ujao utakaofanyika Oktoba 25 mwaka huu, watahakikisha wanashinda kwa kishindo kwa kuchukua viti vingi vya udiwani na ubunge katika majimbo ya Mbinga vijijini na mjini, hivyo wamewaomba wananchi waendelee kuwaunga mkono siku uchaguzi huo utakapofanyika ili waweze kufikia malengo husika.

Kenan Mkuzo ambaye ni Mwenyekiti wa chama hicho wilayani Mbinga, alisema hayo alipokuwa akihutubia mamia ya wananchi waliokusanyika kusikiliza mkutano wa hadhara uliofanyika jana kwenye viwanja vya soko kuu, mjini hapa.

“Ndugu zangu wanambinga naomba niwaeleze, wakati wa kuburuzwa sasa umepita tunahitaji tupate viongozi bora watakaokaa madarakani na kuweza kupigania maendeleo yetu kwa moyo wa dhati, hatuhitaji viongozi lege lege ambao watalifikisha taifa hili mahali pabaya”, alisema Mkuzo.


Mkutano huo ambao ulihudhuriwa na watu wengi na kufunika viwanja hivyo, Mkuzo aliwaeleza wananchi kwamba kuna kila sababu kukichagua CHADEMA kwa kukipigia kura nyingi kwa nafasi ya Udiwani, Ubunge na Rais  ili kiweze kushika madaraka ya nchi hii na kuweza kuleta maendeleo kwa manufaa ya kizazi cha sasa na baadaye.

Pia katika mkutano huo, Wenyeviti wawili wa vitongoji kutoka tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) walikihama chama hicho na kuhamia CHADEMA ambao ni; Steven Mateso kutoka kitongoji cha Mbinga mjini A na John Kabuyuka wa kitongoji cha Masumuni vyote vya mjini hapa.

Wenyeviti hao kwa nyakati tofauti mara baada ya kukabidhiwa kadi za CHADEMA waliapa kwamba, watahakikisha wanashirikiana kwa pamoja kwenye uchaguzi mkuu ujao chama hicho kinapata viti vingi vya uongozi.


Vilevile Katibu Mwenezi wa kata ya Lukarasi, Nestory Kapinga Mbinga vijijini naye alirudisha kadi ya CCM na kuhamia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo, huku akisema kuwa amechukua maamuzi hayo kutokana na kuchoshwa na sera za Chama cha Mapinduzi.

No comments: