Tuesday, August 25, 2015

WAANDISHI WA HABARI WATAKIWA KUJIENDELEZA KIELIMU

Baadhi ya Waandishi wa habari mkoani Ruvuma, wakiwa katika picha ya pamoja nje ya ukumbi wa Ushirika mjini Songea mara baada ya kumaliza mkutano wao wa kuwachagua viongozi watakaoingoza Klabu ya waandishi hao, mkoani humo.
Na Kassian Nyandindi,
Songea.

ANDREW Kuchonjoma ambaye ni Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari mkoani Ruvuma (RPC) amewataka wanachama wake ndani ya klabu hiyo, kujiendeleza kielimu katika tasnia ya habari ili waweze kufanya kazi zao kwa urahisi, katika ulimwengu huu wa sayansi na tekinolojia.

Sambamba na hilo alieleza kuwa kuna kila sababu kwa mwandishi wa habari kuzingatia maadili ya taaluma hiyo, wakati wa kutekeleza majukumu ya kazi zake ya kila siku hasa kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu, ili kuweza kuepukana na matatizo au migogoro inayoweza kujitokeza baadaye.

“Ndugu zangu kusoma ni jambo muhimu sana ambalo tunapaswa kulipatia kipaumbele, hapa Ruvuma kuna chuo cha habari ambacho nawashauri wenzangu tujiunge na tuweze kupata fursa ya kujiendeleza kielimu tusiishie kukaa tu bila kuwa na mawazo mapya ya kujiendeleza kielimu, katika taaluma hii tuliyonayo”, alisema Kuchonjoma.


Kuchonjoma ambaye pia ni mwandishi wa habari mkongwe, alisema hayo alipokuwa akizungumza na wanachama wa RPC mara baada ya kufanyika mkutano mkuu wa uchaguzi wa viongozi wa chama hicho, uliofanyika hivi karibuni kwenye ukumbi wa Ushirika uliopo mjini Songea.

Aidha kwa upande wake msimamizi mkuu wa uchaguzi huo, Mathew Ngalimanayo ambaye ni Katibu mtendaji wa mashirika yasiyokuwa ya kiserikali wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, aliwapongeza waandishi wa habari wa mkoa huo kwa kujenga ushirikiano na kuendeleza mchakato wa kuanzisha redio ambayo itamilikiwa na wanachama wa chama hicho mara itakapoanza kurusha mawimbi yake hewani.

“Nimejifunza ninyi kweli mnao ushirikiano wa kutosha na katiba yenu mnaisimamia ipasavyo katika shughuli za maendeleo ndani ya chama chenu, nawaomba endeleeni kuwa wabunifu ninahakika mtafikia mahali pazuri kwani kila jambo linamchakato wake, kinachotakiwa hapa ni kuendeleza mshikamano ili mfikie malengo yenu mliyojiwekea”, alisema Ngalimanayo.

Pamoja na mambo mengine viongozi waliochaguliwa ambao watakiongoza Chama cha waandishi wa habari mkoani humo, katika kipindi cha miaka mitatu ambao ni; kwa nafasi ya Mwenyekiti ilichukuliwa na Andrew Kuchonjoma, makamu Mwenyekiti, Marietha Msembele, Katibu mtendaji, Andrew Chatwanga, Katibu mtendaji msaidizi Ngaiwona Nkondola, Mweka hazina Joyce Joliga na msaidizi wake ni Alpius Mchucha.


Wajumbe wa kamati tendaji ni Kassian Nyandindi, Joseph Mwambije, Mpenda Mvula na Geofrey Nillahi.

No comments: