Thursday, August 13, 2015

VURUGU ZAENDELEA KUJITOKEZA KUPINGA KURUDIWA UCHAGUZI KURA ZA MAONI MBINGA VIJIJINI

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Jakaya Mrisho Kikwete.
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

WANACHAMA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Mbinga vijijini mkoani Ruvuma, wameandamana kuelekea kwenye Ofisi za chama hicho wakipinga kurudiwa uchaguzi kura za maoni katika kata ya Kihangimahuka na Ruanda wilayani hapa, kwa madai kwamba kufanya hivyo kunalenga kumbeba mgombea mmojawapo ambaye aliangukia pua katika uchaguzi huo uliofanyika hivi karibuni, Agosti Mosi mwaka huu.

Tukio hilo la aina yake limetokea leo majira ya asubuhi katika makao makuu ya Ofisi za CCM wilaya, ambapo wanachama hao walionekana kujawa jazba huku wakidai maamuzi ya kurudiwa kwa uchaguzi huo sio sahihi na kwamba huenda ukakigawa chama na kuzua migogoro miongoni mwa wanachama.

Hali ya kata hizo ambako uchaguzi uliamriwa urudiwe na Kamati kuu ya chama hicho Taifa, hivi sasa imeendelea kuwa tete ambapo wanachama waliopo katika maeneo hayo nao wameandamana kupinga uchaguzi huku wengine wakitishia kukihama chama.


Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa kata ya Ruanda John Ndimbo alisema kuwa wao wanachokifahamu viongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga, ndio wamekuwa chanzo cha migogoro kutokana na kumbeba mgombea, Gaudence Kayombo ambaye alishindwa kwenye kinyang’anyiro cha kura za maoni zilizofanyika hivi karibuni.

“Baadhi ya watumishi wa Halmashauri jana Agosti 12 mwaka huu, wameonekana majira ya usiku wakipita nyumba kwa nyumba kushawishi wanachama wampigie kura Kayombo huku wakidaiwa kugawa fedha shilingi 5,000 na vifaa vya ujenzi kama vile bati, mifuko ya saruji na nondo jambo hili binafsi linanishangaza sana sisi tunachotambua uchaguzi kura za maoni ulikwisha fanyika”, alisema Ndimbo.

Naye Hallad Ndimbo ambaye ni Katibu wa CCM kata ya Kihangimahuka, alisema taarifa za kurudiwa kwa uchaguzi huo zinamshangaza na kwamba yeye hatashiriki katika zoezi hilo ambalo kimsingi linaonekana kushinikizwa na baadhi ya vigogo wachache, ngazi ya Halmashauri ya wilaya hiyo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi wilayani humo, Christantus Mbunda alifafanua kuwa haki haijatendeka kuhusiana na kurudia kwa uchaguzi huo, kutokana na wagombea wengine kutokuwepo huku akiongeza kwamba ili haki itendeke ni lazima wote kwa pamoja wawepo, ili kuondoa malalamiko yasiyokuwa ya lazima.

Mbunda alieleza kuwa yeye binafsi anachofahamu uchaguzi ulikwishafanyika kwa haki ambapo kwa kata hizo mbili za Kihangimahuka na Ruanda, baadhi ya watu waliingilia akiwemo yeye mwenyewe mgombea Kayombo na kuharibu mfumo wa matokeo ya kura za maoni, ambayo yalikwisha pigwa na wapiga kura.

“Kama kurudia uchaguzi ni vyema ukarudiwa jimbo zima na sio kwa kata mbili ambako anatokea mgombea, tunaiomba kamati kuu ya CCM Taifa kwa nia njema kabisa na kwa manufaa ya chama chetu itende haki kwa wagombea wote”, alisema Mbunda.

Aliongeza kuwa Chama Cha Mapinduzi ni kizuri na watanzania wengi wanakipenda, ila tu kuna watu wachache ambao wanamalengo ya kukiharibu ikiwemo kung’anga’nia madarakani, hata kama wanachama na wananchi hawawataki.

Mbunda alisema wakati umefika kwa wale wote wenye tabia ya kung’ang’ana na madaraka, waache tabia hiyo badala yake wakubali matokeo kwani kufanya hivyo kutasaidia kujenga chama na kuondokana na kero mbalimbali, zinazosababisha migongano baina ya wanachama na viongozi.

No comments: