Sunday, February 19, 2017

WAJUMBE WA BODI MBINGA WALIMU SACCOS WASWEKWA RUMANDE WAKITUHUMIWA KUIBA MILIONI 540,704,572

Askari Polisi wa Kituo kikuu cha Polisi wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma ambaye jina lake halikuweza kupatikana mara moja, akimuongoza mmoja kati ya watuhumiwa wa fedha za Mbinga Walimu SACCOS iliyopo wilayani humo, Edmund Hyera baada ya kuamriwa na Mrajisi msaidizi wa vyama vya ushirika mkoani hapa, Biezel Malila wakamatwe jana kwenye mkutano maalumu wa Wanachama wa SACCOS hiyo uliofanyika mjini hapa ambapo inadaiwa kuwa yeye na watuhumiwa wenzake walishiriki kuiba shilingi milioni 540,704,572. (Picha na Muhidin Amri)
Na Kassian Nyandindi,       
Mbinga.

WAJUMBE wa bodi ya Kamati ya usimamizi Chama cha ushirika Mbinga Walimu SACCOS iliyopo wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wamekamatwa na kuwekwa mahabusu wakituhumiwa kuiba shilingi milioni 540,704,572 za wanachama wa chama hicho cha ushirika na kusababisha hasara kubwa kwa chama kushindwa kujiendesha kwa manufaa ya wanachama.

Aidha hatua hiyo ya kukamatwa kwa Wajumbe hao ilitolewa na Mrajisi msaidizi wa vyama vya ushirika mkoani humo, Biezel Malila baada ya kusomwa taarifa ya ukaguzi juu ya mwenendo wa chama hicho cha ushirika ambayo ilibainisha wizi wa fedha hizo katika mkutano mkuu maalumu wa wanachama, uliofanyika Februari 18 mwaka huu kwenye ukumbi wa Jumba la maendeleo mjini hapa.

“Kwa masikitiko makubwa ndugu zangu wanachama mliohudhuria mkutano huu naomba niwaeleze kwamba mwenendo wa chama hiki sio mzuri unatia kichefuchefu, chama kina hali mbaya kina hati chafu ya ukaguzi kwa kuwa Wajumbe wa bodi hii wameshiriki kwa namna moja au nyingine kukiuka taratibu za uendeshaji wa chama hiki, hivyo wanapaswa kuwajibika kwa mujibu wa sheria na taratibu husika za vifungu vya uendeshaji wa vyama vya ushirika”, alisema Malila.

Mrajisi huyo wa vyama vya ushirika mkoa wa Ruvuma alifafanua kuwa fedha hizo ambazo Wajumbe hao wanadaiwa kuiba na kujinufaisha kwa matakwa yao binafsi zilitokana na baki ya mikopo shilingi milioni 174,915,794 hisa, akiba na amana shilingi milioni 363,873,778 na mikopo ambayo waliitengeneza bila kufuata taratibu husika walichota shilingi milioni 1,915,000.


Alieleza kuwa mpaka sasa ni Wajumbe kumi na nne ndio waliohusika kuiba fedha hizo ambazo ni za wanachama wa Mbinga Walimu SACCOS ambapo kati ya hao waliokamatwa na kuwekwa mahabusu ni wanne tu ambao ni Sostenes Ndunguru ambaye ni Meneja, Prosper Mbepera ni Mhasibu, Stephen Komba mjumbe kamati ya usimamizi na Edmund Hyera ambaye ni mjumbe wa bodi.

Alifafanua kuwa Wajumbe kumi wamekimbia hawajulikani walipo ambapo taarifa zao zimeripotiwa Kituo kikuu cha Polisi wilaya ya Mbinga na kwamba wanatafutwa ili waweze kujibu tuhuma hizo zinazowakabili ambao ni Emmanuel Kapinga Mwenyekiti, Kenneth Ndunguru, John Komba, Peter Challe, Batson Mpogolo, Osmund Komba, Wille Mkwene, Marion Nchillas, Materinus Ndunguru na Tabu Mshani ambao wote nao walikuwa ni Wajumbe wa bodi katika SACCOS hiyo.

“Hawa waliotoroka kufuatia kuwepo kwa kesi hii ya ubadhirifu wa fedha hizi, madai yao yamefunguliwa Kituo kikuu cha Polisi Mbinga, tunawatafuta popote pale walipo ili waweze kukamatwa na kujibu tuhuma hizi zinazowakabili mbele yao na kila mtu atabeba mzigo wake”, alisisitiza Malila.

Malila aliongeza kuwa fedha hizo ambazo zililenga kuwanufaisha wanachama kwa mtindo wa kukopeshana cha kushangaza Wajumbe hao wamejinufaisha kwa matakwa yao binafsi, hivyo wanatakiwa kuzilipa kwa mujibu wa kifungu namba 55 cha sheria ndogo namba 13 ya ushirika namba 6 ya mwaka 2013.

Kadhalika kufuatia kuwepo kwa tukio hilo Mrajisi huyo ametoa wito kwa viongozi na watendaji wa vyama vya ushirika mkoa wa Ruvuma, akiwaonya kuacha vitendo vya wizi wa fedha na mali za ushirika na kwamba ofisi yake itaendelea kuchukua hatua za kuwafungulia mashtaka wale wote watakaobainika kushiriki katika upotevu wa mali za ushirika.

Vilevile Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Zubery Mwombeji amethibitisha kuwepo kwa tukio hilo ikiwemo kukamatwa kwa watuhumiwa hao wanne, huku akifafanua kuwa wanaendelea kuhojiwa kutokana na tuhuma zinazowakabili na hao wengine kumi waliobakia ambao wamekimbia hawajulikani walipo Jeshi hilo linaendelea kuwasaka popote pale ili waweze kuwakamata na kujibu tuhuma hizo zinazowakabili.


Awali wakichangia hoja kwa nyakati tofauti katika mkutano huo wanachama wa SACCOS hiyo waliunga mkono jitihada hizo zilizochukuliwa na Mrajisi huyo wa vyama vya ushirika mkoani hapa, huku wengine wakidai kuwa wamesikitishwa kwa taarifa hizo ambazo ni utovu mkubwa wa nidhamu uliofanyika ndani ya chama chao juu ya matumizi mabaya ya fedha za wanachama.

Percy Komba ambaye ni mmoja kati ya wanachama wa ushirika huo alisema kuwa taarifa hiyo ya mkaguzi ambayo imesomwa mbele yao inaonesha kuwa na madudu mengi ya ubadhirifu wa fedha na dosari za kiutendaji, hivyo kwa uchungu walionao wanachama kuna kila sababu kwa viongozi wao kuchukuliwa hatua za kisheria ili iwe fundisho kwa wengine.

Naye Renatus Nambombe ambaye ni mwananchama wa ushirika huo aliongeza kwa kusema kuwa tukio hilo wanalilinganisha na msiba mkubwa ambao umewapata na hawakutegemea kama yangeweza kutokea mambo hayo.

“Kwa kilio hiki kilichotupata hawa watuhumiwa wanastahili kabisa kukamatwa  na kutiwa pingu mikononi ili wafikishwe Mahakamani, kwani inasikitisha sana na kutuongezea uchungu mkubwa katika maisha yetu”, alisema Nambombe.

Pamoja na mambo mengine chama hicho cha ushirika kinaundwa na wanachama ambao ni watumishi wa serikali kutoka katika halmashauri ya mji wa Mbinga, wilaya ya Mbinga na Nyasa ambapo makao makuu ya ofisi zake yapo Mbinga mjini.

Katika mkutano huo hatua iliyofuata ilikuwa ni ya kuvunja bodi ya Chama hicho cha ushirika Mbinga Walimu SACCOS kufuatia kuwepo kwa matatizo hayo ya wizi wa fedha za wanachama na kwamba, waliteuliwa Wajumbe watano wa bodi ya mpito mpaka utakapofanyika uchaguzi mkuu wa kuwachagua Wajumbe wengine watakaoweza kuongoza ushirika huo.

Wajumbe hao walioteliwa kuongoza watadumu kwa muda usiozidi mwaka mmoja ambao ni Vitalis Mapunda ambaye ni Mwenyekiti, Judith Komba, Sota Ndunguru, Michael Simbo na Silvester Msuha ambao wote ni wajumbe wa mpito kamati ya usimamizi.

Awali hivi karibuni nao Watumishi saba wanaotoka katika halmashauri hizo wilayani humo ambao pia ni Wajumbe wa bodi ya Chama cha ushirika Mbinga Kurugenzi SACCOS iliyopo mkoani hapa, walikamatwa Januari 21 mwaka huu waliwekwa mahabusu na kufikishwa Mahakamani wakituhumiwa kuiba shilingi milioni 500 za wanachama wa chama hicho cha ushirika.

Kukamatwa kwao na kufikishwa katika mkono wa sheria kulitokana pia na Mrajisi huyo wa vyama vya ushirika mkoa wa Ruvuma kueleza kwamba fedha hizo ambazo Wajumbe hao wanadaiwa kujinufaisha kwa matakwa yao binafsi zilitokana na mkopo wa shilingi milioni 500 uliotolewa na benki ya CRDB kwa ajili ya kukopeshwa wanachama lakini cha kushangaza waliamua kuzitumia kinyume na taratibu husika.


Hata hivyo watuhumiwa hao saba ni Zackaria Lingowe, Emmanuel Mwasaga, Alex Kalilo, Jamima Challe, Stella Mhagama, Lucas Nchimbi, Mhadisa Meshack na kwamba mpaka sasa shtaka lao limefikishwa katika Mahakama ya Hakimu mkazi Mfawidhi mkoa wa Ruvuma ambapo litatajwa tena Marchi 7 mwaka huu.

No comments: