Sunday, February 12, 2017

ASHIKILIWA NA POLISI KWA TUHUMA YA KUMUUA MDOGO WAKE

Na Kassian Nyandindi,     
Songea.

JESHI la Polisi mkoani Ruvuma linamshikilia Omary Likande (32) ambaye ni mkazi wa kijiji cha Msechela wilayani Tunduru mkoani humo, kwa tuhuma ya kumuua mdogo wake Unda Likande (23) kwa kumchoma na kitu chenye ncha kali shingoni.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Zubery Mwombeji alisema kuwa tukio hilo lilitokea Februari 7 mwaka huu majira ya mchana katika kitongoji cha Mkalala kilichopo katika kijiji cha Msechela tarafa ya Namasakata wilayani humo.

Mwombeji alisema kuwa siku hiyo ya tukio inadaiwa kuwa Unda aliuawa kwa kukatwa shingoni na kaka yake, Omary Likande wakati baba yao alipokuwa ametoka kwenda kutafuta chakula.


Alifafanua kuwa tukio hilo lilitokea kwenye kibanda ambacho kipo katikati ya shamba la wazazi wao ambapo Omary baada ya kumuua mdogo wake aliendelea kubaki kwenye eneo hilo mpaka baba yao alipofika na kuona mtoto wake mmoja akitokwa na damu nyingi shingoni.

Alisema kuwa baadaye baba yao alipoona hivyo alitoa taarifa kwa uongozi wa serikali ya kijiji ambao nao ulitoa taarifa kwenye Kituo kikuu cha Polisi wilayani Tunduru na askari walipowasili kwenye eneo la tukio wakiwa wameongozana na daktari ambaye alithibitisha kuwa Unda Likande amefariki dunia kwa kuchomwa na kitu hicho chenye ncha kali.


Jeshi hilo la Polisi limesema kuwa uchunguzi wa awali umebaini kuwa mtuhumiwa Omary Likande ana tatizo la muda mrefu la ugonjwa wa akili ambao huenda ukawa ndiyo chanzo cha tukio hilo.

No comments: