Sunday, February 19, 2017

WILAYA YA MBINGA MKOANI RUVUMA YAONGOZA KWA KILIMO CHA BANGI

Na Kassian Nyandindi,      
Mbinga.

IMEELEZWA kuwa katika mkoa wa Ruvuma wilaya ya Mbinga mkoani humo imekuwa ikiongoza kwa kilimo cha bangi, hivyo serikali itaendelea kupambana na watu wanaohusika na uzalishaji wa zao hilo kwa kuwachukulia hatua za kisheria ikiwemo kuwafikisha Mahakamani.

Aidha wananchi wametakiwa kutoa ushirikiano mara kwa mara kwa viongozi wa ngazi ya vijiji, kata hadi wilaya katika utoaji wa taarifa ni wapi kumekuwa na mashamba ambayo yamekuwa yakitumika kuzalisha zao hilo.

Mkuu wa wilaya hiyo, Cosmas Nshenye alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na Madiwani pamoja na wananchi kwenye kikao cha kujadili mapendekezo ya mpango wa bajeti ya maendeleo halmashauri ya mji wa Mbinga kwa mwaka wa fedha wa 2017/2018 kilichofanyika kwenye ukumbi wa Jumba la maendeleo mjini hapa.


“Vita ya madawa ya kulevya ni kubwa hata hapa kwetu ipo, tatizo hili tayari wengine tumewafikisha Mahakamani na wengine bado tunawachunguza natoa wito kwenu sisi sote ni wadau katika kupambana nalo”, alisisitiza Nshenye.

Nshenye alifafanua kuwa anatambua kwamba Madiwani, Watendaji wa vijiji na kata katika maeneo yao wamekuwa wakifahamu watu wanaohusika na usambazaji wa madawa hayo ya kulevya, hivyo wanapaswa kutoa taarifa hizi kwenye vyombo vya dola ili hatua ziweze kuchukuliwa mapema.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kikao hicho kufanyika naye diwani wa kata ya Mpepai, Benedict Ngwenya alieleza kuwa bangi katika wilaya ya Mbinga imekuwa ikizalishwa hasa katika kata yake kutokana na kata hiyo kuwa na mapori makubwa ambayo yamepakana na hifadhi ya wanyama ya Liparamba.


Ngwenya aliongeza kuwa pia katika hifadhi hiyo baadhi ya watu ambao ndio wanaendekeza kilimo cha zao hilo wamekuwa wakiingia ndani ya msitu wa hifadhi na kulima bangi na kwamba ameiomba serikali ifanye oparesheni maalumu ya kuchunguza kwa kina na kuwabaini ili hatimaye kuteketeza kabisa kilimo hicho kisiweze kuendelea na kuathiri jamii hasa vijana ambao ndiyo tegemeo la kukuza uchumi kwa faida ya kizazi cha sasa na baadaye.

No comments: