Monday, February 27, 2017

VIONGOZI WA VYAMA VYA SIASA WATAKIWA KUJENGA USHIRIKIANO

Na Dustan Ndunguru,     
Mbinga.

MWENYEKITI wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Ambrose Nchimbi  amewataka viongozi wa kisiasa na watendaji katika maeneo mbalimbali wilayani humo, kujenga ushirikiano katika kutekeleza majukumu yao na kuacha kuendekeza malumbano badala yake wasimamie vyema ujenzi wa miradi ya wananchi ili iweze kukamilika kwa wakati na viwango vinavyotakiwa.

Akizungumza na mwandishi wetu, Nchimbi alisema kuwa baadhi ya maeneo wilayani humo miradi ya wananchi ya maendeleo imekwama haijakamilika kwa wakati uliopangwa kutokana na tabia ya viongozi kuendekeza malumbano hasa yanayochochewa na viongozi wa vyama vya siasa.

Alivinyoshea kidole vyama vya upinzani kutokana na tabia ya viongozi wake kuwakatisha tamaa wananchi kwa kuwadanganya kuwa serikali imewasahau kitu ambacho sio cha kweli.


Alifafanua kuwa Madiwani wa vyama hivyo wamekuwa mstari wa mbele kuwadanganya wananchi, wakiwaelekeza kwamba kwenye maeneo yao wasichangie nguvu zao katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo jambo ambalo alisema ni upotoshaji ambapo halipaswi kuungwa mkono kwani kitendo hicho ni sawa na kuhamasisha umaskini uendelee kuwepo miongoni mwa jamii.

Nchimbi alisema serikali imekuwa ikipeleka fedha nyingi za utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika halmashauri zake, lakini kama viongozi hawataonesha ushirikiano mzuri upo uwezekano mkubwa wa kutotekelezeka kwa miradi hiyo.


“Wakati umefika kwa viongozi wa ngazi zote kushirikiana na kufanya kazi za kusimamia utekelezaji wa miradi hii ya maendeleo ambayo imeibuliwa na wananchi ili iweze kukamilika kwa wakati na viwango vinavyotakiwa”, alisisitiza Nchimbi.

No comments: