Sunday, February 26, 2017

KITURA SEKONDARI HAINA MWALIMU WA HESABU NA FIZIKIA


Na Kassian Nyandindi,    
Mbinga.

SHULE ya Sekondari Kitura iliyopo katika kata ya Kitura wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, haina mwalimu wa somo la Hisabati na Fizikia tangu kuanzishwa kwake mwaka 2007 jambo ambalo limekuwa likisababisha wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo kutosoma kabisa masomo hayo muhimu kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne.

Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Cosmas Nshenye.
Kaimu Mkuu wa shule hiyo, Stanslaus Mapunda alisema hayo juzi wakati wa ziara ya Madiwani ambao ni Wajumbe wa Kamati ya uongozi na mipango ya halmashauri ya wilaya hiyo, iliyokuwa ikiongozwa na Mwenyekiti wake Ambrose Nchimbi.

Mapunda alisema kuwa licha ya kulifikisha tatizo hilo katika mamlaka husika kwa muda mrefu hakuna utekelezaji uliofanyika na kwamba mpaka sasa pia hakuna ufumbuzi uliofikiwa juu ya utatuzi wa tatizo hilo hivyo wanalazimika kufundisha masomo mengine tu jambo ambalo limekuwa likisababisha watoto hao kutopata fursa nzuri ya kujisomea.

Kwa upande wake Mratibu elimu kata, Nikodem Hyera alisema kuwa bado wataendelea kufuatilia walimu hususani hao wa masomo hayo mawili ambayo hayana walimu ili kuepukana na tatizo hilo ambalo limedumu kwa miaka kumi sasa bila kupatiwa ufumbuzi wa kudumu.

Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga, Nchimbi alisema kuwa ipo changamoto kubwa ya upungufu wa walimu wa masomo ya hesabu na sayansi hivyo serikali wilayani humo itahakikisha inawasiliana na mamlaka husika ili kuweza kuona ni namna gani tatizo hilo linapatiwa ufumbuzi kwa kuwapelekea walimu wa masomo hayo.

“Tatizo la walimu wa masomo haya halipo huku kwetu pekee bali ni la nchi nzima hivyo pamoja na tatizo hili kuwepo hapa kwetu, lazima tuhakikishe tunalimaliza hata kama tutapata mwalimu mmoja atakayeweza kufundisha masomo haya mawili”, alisema Nchimbi.

Hata hivyo Nchimbi alisema kuwa kuwepo kwa changamoto hiyo kunawafanya hata wazazi kushindwa kuwahamasisha watoto wao wapende kusoma masomo ya sayansi na kwamba licha ya tatizo hilo, kwa wale ambao wamebahatika shule zao kuwa na walimu wanaofundisha masomo hayo wanapaswa kuhakikisha kuwa wanasoma kwa bidii ili hatimaye wataalamu wanaotokana na masomo hayo waweze kupatikana kwa urahisi kama vile waganga na wataalamu wa afya.

No comments: