Saturday, February 11, 2017

BARAZA LA MADIWANI MBINGA LAWAFUKUZA KAZI WATUMISHI WAKE

Na Kassian Nyandindi,     
Mbinga.

BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma limewafukuza kazi baadhi ya watumishi wake, kutokana na makosa mbalimbali yakiwemo ya utoro kazini na kuisababishia halmashauri hiyo hasara ya shilingi milioni 46,680,000.

Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Ambrose Nchimbi akitangaza jana kufukuzwa kazi kwa watumishi hao katika baraza hilo alisema kuwa wamefikia maamuzi hayo baada ya baraza hilo kuketi kama kamati kwa muda wa masaa matatu kujadili suala hilo na kufikia maamuzi hayo, ambayo alieleza kuwa yatakuwa fundisho kwa watumishi wengine wenye tabia kama hiyo.

Nchimbi alisema kuwa waliofukuzwa kazi ni Mosta Ndunguru ambaye ni Afisa tabibu na Bapara Mwang'ombe Mhudumu wa afya ambapo wote kwa pamoja wamefukuzwa kwa makosa ya utoro kazini.


Aliwataja wengine waliofukuzwa kazi kwa kosa la kuisababishia halmashauri hiyo ya Mbinga hasara ya shilingi milioni 46,680,000 kuwa ni watumishi wawili ambao ni maofisa misitu wasaidizi, Kelvin Haulle na Ally Almasi.

Katika hatua nyingine Mwenyekiti huyo aliongeza kuwa Anyitike Kasongo ambaye alikuwa ni Kaimu Mhandisi idara ya ujenzi, amevuliwa madaraka hayo kutokana na kushindwa kusimamia kikamilifu miradi ya ujenzi wa nyumba za walimu katika kata ya Kitura wilayani humo.


Vilevile aliwataja wengine ambao nao walikuwa wamesimamishwa kazi kutokana na sababu mbalimbali na baraza hilo limewarejesha kazini kuwa ni Ahsante Luambano aliyekuwa Mratibu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), Said Almasi ambaye ni Fundi sanifu idara ya ujenzi, Kebrina Tembo Afisa mtendaji wa kata, Cosmas Mmasai, Mhasibu daraja la pili na Emmanuely Kapinga Afisa utumishi ambaye amefutiwa mashtaka yaliyokuwa yakimkabili ya uzembe kazini.

No comments: